VIDEO: Rais Magufuli atangaza kuhamia Dodoma

Saturday October 12 2019

 

By Gerson Msigwa, Ikulu

Dodoma. Rais wa Tanzania,  John Magufuli ametangaza kuhamia Dodoma kuanzia leo Jumamosi Oktoba 12, 2019.

Rais Magufuli amesema hayo mara baada ya kumaliza kujiandika katika orodha ya wapiga kura ya serikali za mitaa akiwa na mkewe Mama Janeth Magufuli.

Wawili hao wamejiandika katika kituo cha Sokoine kilichopo katika Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma baada ya kuwasili wakitoka mkoani Katavi.

Baada ya kujiandikisha, Rais Magufuli amesalimiana na wananchi wa Chamwino waliokuwa wamejitokeza kujiandikisha katika kituo hicho na kuwaeleza kuwa pamoja na kwamba miundombinu ya Ikulu ya Chamwino bado haijakamilika yeye ameshahamia Dodoma.

“Mimi nilikuwa Katavi, nimeamua kuja kujiandikisha nyumbani kwa sababu hapa ndio nyumbani kwangu, na nimeshakuja rasmi hapa, kwa hiyo kila siku tutakuwa tunaonana hapa, ndio maana nimeona nije nijiandikishe mimi pamoja na mke wangu” amesema Rais Magufuli.

Uamuzi huo wa Rais Magufuli umehitimisha ahadi yale aliyoitoa huko nyuma ya kuhamia Dodoma kwani tayari Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wizara na taasisi mbalimbali zilikwisha kuhamia Dodoma.

Advertisement

Kuhusu uchaguzi, Rais Magufuli amewataka Watanzania kuendelea kujitokeza katika vituo vya kujiandikisha vilivyopo nchi nzima ili Novemba 14, 2019 waweze kutumia haki yao ya kikatiba ya kuwachagua viongozi wa Serikali za Mitaa watakaowana wanafaa.

Aidha, Rais Magufuli amewapongeza waandishi wa habari wa Mkoa wa Dodoma waliofika katika kituo hicho kwa kutekeleza majukumu yao ya uandishi wa habari na amewasisitiza kuendelea kutimiza majukumu hayo kwa weledi na kwa kutanguliza maslahi ya Taifa.

Baadaye, Rais Magufuli amewaalika waandishi wa habari hao na kula nao chakula cha mchana, nyumbani kwake katika Ikulu ya Chamwino.

Advertisement