VIDEO: Rais Magufuli atoa neno vitambulisho vya uraia

Muktasari:

  • Rais wa Tanzania, John Magufuli amemtaka mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Dk Arnord Kihaule kufuatilia shughuli za utolewaji wa vitambulisho vya uraia nchi nzima.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amemtaka mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Dk Arnord Kihaule kufuatilia shughuli za utolewaji wa vitambulisho vya uraia nchi nzima.

Ametoa agizo hilo leo Jumatano Novemba 20, 2019 mkoani Morogoro baada ya wananchi wa eneo la Msamvu kumueleza adha wanazokumbana nazo wakati wa kujiandikisha kupata vitambulisho hivyo.

Magufuli mbali na kumuagiza Dk Kihaule kwenda Morogoro kutatua changamoto hiyo, amesema tatizo linalowakabili wakazi hao huenda likawa linawakumba wananchi wengine katika maeneo mbalimbali nchi.

Vitambulisho hivyo vina umuhimu mkubwa kwa kuwa ili uweze kusajili laini ya simu ni lazima uwe na kitambulisho hicho kinachotolewa na Nida.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Desemba 31, 2019 ndio mwisho wa usajili wa laini za simu kwa alama za vidole na hadi Agosti, 2019 laini milioni 5.2 ndio zilikuwa zimesajiliwa kati ya laini milioni 44.2.

Kitambulisho hicho pia ndio hutumika kusajili kampuni, kuomba hati ya kusafiria na kupata cheti cha kuzaliwa.

Baada ya wananchi kumueleza changamoto wanazokumbana nazo, Magufuli alimpigia simu Dk Kihaule, “nipo Morogoro hapa nimeelezwa tatizo la Nida, mna ofisi moja tu Mkoa wa Morogoro kwa nini? Mbona watu wa Kilosa wanakuja hapa wanapata shida.”

“Sasa nisikilize mkurugenzi uko wapi uko Dar? Ondoka sasa hivi uje hapa Morogoro ushughulikie hili tatizo la Nida na ninataka watu walioko wilayani wasije hadi mkoani uje kutatua hili tatizo la Nida.”

“Leo uje hapa Morogoro ukae na Mkuu wa Mkoa na mkuu wa Wilaya ujipange ofisi yako izunguke katika wilaya zote ili wananchi wapate vitambulisho haraka.”

Kiongozi mkuu huyo wa nchi amesema huenda tatizo linalowakabili wakazi wa Morogoro lipo katika maeneo mengine, kutamaka mkurugenzi huyo kufuatilia mikoa yote.

“Inawezekana matatizo yapo Tanzania nzima na sio Morogoro pekee mzunguke katika wilaya zote ili wananchi wapate huduma haraka,” amesema kiongozi mkuu huyo wa nchi.

Baada ya maelekezo hayo Magufuli amesema, “sasa ndugu zangu wa Morogoro nimemuagiza mkurugenzi mkuu wa Nida atakuja hapa leo na mimi atanipa majibu ndani ya siku tatu na atanipa utaratibu kwa nchi nzima.”