Ripoti: Wanaume wanajiua zaidi kuliko wanawake

Thursday September 12 2019

 

Geneva, Uswisi. Ripoti mpya ya Shirika la Afya Duniani (WHO), imesema kuwa kila sekunde 40 kuna mtu anajiua duniani.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, karibu watu 800,000 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na kujiua idadi ambayo ni kubwa zaidi ukilinganishwa na vifo vinavyotokana na sababu mbalimbali ikiwamo vita, wanaouliwa na magonjwa.

Ripoti hiyo inasema kuwa kujiua kunashika nafasi ya pili kusababisha vifo vingi miongini mwa vijana wenye umri kati ya miaka 15 na 29.

Hata hivyo, katika ripoti hiyo, WHO inasema viwango vya kujiua duniani vimepungua kwa kiasi fulani kati ya mwaka 2010 na 2016 ingawa idadi ya vifo imeendelea kuwa pale pale kutokana na ongezeko la idadi ya watu duniani.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema katika taarifa yake kuwa licha ya hatua mbalimbali zinazochukuliwa bado kuna mtu anafariki kila sekunde 40 kutokana na kujiua kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2019.

Alisema takwimu za mwaka 2016, ambazo ndiyo wa mwisho kutolewa zilionyesha kwa kila watu 100,000 kulikuwa na vifo 10.5 vinavyotokana na kujiua.

Advertisement

“Kwa ujumla viwango vya kujiua duniani vimepungua kwa karibu asilimia 10 kuanzia 2010 hadi 2016, lakini kanda ya Marekani imeonesha kuongezeka kwa viwango hivyo kwa asilimia sita katika kipidi cha miaka sita.

Ripoti hiyo ya WHO inasema idadi ya mataifa yaliyo na mikakati ya kuzuia watu kujiua imeongezeka katika kipindi cha miaka mitano tangu kuchapishwa kwa ripoti ya kwanza ya dunia ingawa bado ni ndogo.

Ripoti hiyo imebainisha viwango vikubwa vya mauaji hutokea katika nchi maskini na ya maendeleo ya kati ambako ndiyo yenye idadi kubwa ya watu na kufatiwa na chi tajiri.

Ripoti hiyo imetaja nchi ya Guyana kuongoza kwa matukio ya kujiua ikifuatiwa na Urusi iliyoshika nafasi ya pili. Mataifa mengine yalioko kwenye orodha hiyo ni pamoja na Lithuania, Lesotho, Uganda, Sri Lanka, Korea Kusini, India na Japan pamoja na Marekani.

Ripoti hiyo pia inbainisha kuwa wanaume ndiyo wanaongoza kwa kujiua ukilinganisha na wanawake ingawa katika mataifa matano pekee ikiwamo Bangladesh, China, Lesotho, Morocco na Myanmar ndiyo wanawake waliongoza kwa kujiua.

Mtaalamu kutoka kitengo cha afya ya akili kutoka shirika hilo, Alexander Fleischmann alisema kuwa mauaji ya kijiua ni tatizo kubwa la afya ya jamii na kutoa wito wa hatua kuchukuliwa kushughulikia tatizo hilo.

"Ni muhimu wakati wote kuzuia vifo vya kujiua kwa watu wanatuzunguka. Inapaswa kuchukuliwa kwa uzito mtu anaposema hataki tena kuishi au kujitoa uhai wake. Kila moja wetu ana jukumu katika kuzuia mauaji ya kujiua. Hivyo sote tunaweza kujitolea kuwasikiliza watu wanaotuzunguka wanapokuwa kwenye huzuni au wanataka msaada wetu.”

Advertisement