Sababu kesi ya Zitto Kabwe kupigwa kalenda

Kiongozi wa chama cha  ACT Wazalendo Zitto Kabwe akitoka katika kesi inayomkabili ya kutoa lugha ya uchochezi mahakama ya kisutu leo picha na Omar  Fungo

Muktasari:

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kuendelea kusikiliza kesi ya uchochezi inayomkabili Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe baada ya kuelezwa kuwa mshtakiwa huyo ambaye ni kiongozi wa chama hicho amefiwa.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kuendelea kusikiliza kesi ya uchochezi inayomkabili Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe baada ya kuelezwa kuwa mshtakiwa huyo ambaye ni kiongozi wa chama hicho amefiwa.

Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga amedai mbele ya Hakimu Mkazi mkuu, Huruma Shaidi kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kusikilizwa.

Wakili wa Utetezi, Peter Kibatala amedai leo Jumatatu Oktoba 7, 2019 kuwa mteja wake amefiwa mkoani Kigoma, anaomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kusikiliza kesi hiyo.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Shaidi ameahirisha shauri hilo hadi Oktoba 22 na 23, 2019 itakapokuja kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.

Tayari mashahidi 12 wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi katika kesi hiyo akiwemo Mkuu wa upelelezi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, John Makungu.

Katika kesi ya msingi, Zitto anakabiliwa na mashtaka matatu ya uchochezi anayodaiwa kuyatenda  Oktoba 28, 2018 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za makao makuu ya chama hicho.