Shahidi aliye masomoni akwamisha kesi ya Zitto

Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe

Muktasari:

Shahidi upande wa mashtaka katika kesi ya uchochezi inayomkabili mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe ameshindwa kufika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutoa ushahidi  ikielezwa kuwa yupo katika masomo.

Dar es Salaam. Shahidi upande wa mashtaka katika kesi ya uchochezi inayomkabili mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe ameshindwa kufika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutoa ushahidi  ikielezwa kuwa yupo katika masomo.

Wakili wa Serikali mkuu, Lilian Ditemba amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Shaidi Huruma kuwa shahidi waliokuwa wakimtarajia amekwenda katika masomo, kuomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya kusikiliza kesi hiyo.

Kufuatia maelezo hayo, hakimu Huruma ameahirisha shauri hilo hadi  Oktoba 7, 8 na 9, 2019 kwa ajili ya kusikilizwa.

Tayari mashahidi 10 wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi katika kesi hiyo.

Katika kesi ya msingi, Zitto ambaye ni kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, anakabiliwa na mashtaka matatu ya uchochezi.

Anadaiwa kutenda makosa hayo Oktoba 28, 2018 katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya ofisi za chama hicho zilizopo Kijitonyama, Dar es Salaam.