Safari za ATCL China zatajwa kuongeza idadi ya watalii Tanzania

Muktasari:

  • Zaidi ya watalii 30,000 kutoka China hutembelea Tanzania kila mwaka huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka baada ya Shirika la Ndege nchini (ATCL) kuzindua safari zake kwenda Guangzhou, China

Dar es Salaam. Zaidi ya watalii 30,000 kutoka China hutembelea Tanzania kila mwaka huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka baada ya Shirika la Ndege nchini (ATCL) kuzindua safari zake kwenda Guangzhou, China.

Hayo yamebainishwa leo Alhamisi Agosti 8, 2019 jijini Dar es Salaam na balozi wa China nchini, Wang Ke katika hafla ya kutangaza washindi wa shindano la kuandika insha kuhusu urafiki kati ya China na Tanzania.

Balozi huyo amesema safari za ndege zikianza zitaongeza mwingiliano na ushirikiano baina ya mataifa hayo ambayo uhusiano wake umefikisha miaka 55 sasa. Amesema nchi hizo zitaendelea kudumisha uhusiano huo kwa ajili ya vizazi vijavyo.

“Utamaduni wa kipekee na utajiri wa asili uliopo hapa Tanzania unapendwa na watu wengi kutoka China. Mwaka huu Air Tanzania inatarajia kuzindua safari zake kati ya Guangzhou na Dar es Salaam, hiyo itachochea zaidi ushirikiano wetu,” amesema Ke.

Kuhusu shindano la uandishi wa insha kuhusu urafiki kati ya China na Tanzania, Ke amesema mashindano kama hayo yanasaidia kuhifadhi historia ya urafiki huo na kuurithisha kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Chama cha Kudumisha Urafiki wa China na Tanzania (TCFPA), Juma Dosa amesema urafiki wa mataifa hayo umejikita katika kuheshimiana, kuaminiana na kuelewana katika njia mbalimbali.

Washindi wanane wa shindano hilo wamepewa zawadi ya fedha na vyeti.

Mshindi wa jumla Humphrey Mrema amesema China ni nchi pekee ambayo ina urafiki wa kweli na Tanzania na hata sasa ndiyo ubalozi ambao umefungua ofisi zake Dodoma baada ya serikali kuhamia.