Sekta ya mawasiliano ya simu ni nguzo muhimu katika kukuza uchumi

Umoja wa Forodha Ulimwenguni (WCO) umesema Tanzania inaweza kunufaika kwa kiasi kikubwa kwa kuwekeza katika teknolojia kwa sababu mabadiliko ya kidijitali yamekuwa chachu kubwa ya kusukuma mbele gurudumu la maendeleo nchini.
Akizungumza jijini Dar Es Salaam, Katibu Mkuu wa WCO, Dk Kunio Mikuriya amesema mbali na faida nyingi, uwekezaji katika teknolojia ya kidijitali ni mojawapo ya njia bora ya kukusanya kodi na mapato ya serikali, hivyo kuwezesha utoaji bora wa huduma nyingine ambazo zinategemea kodi hizo kama vile ujenzi wa miundombinu.
Amesema hivi sasa teknolojia ya kidijitali tayari imeleta matunda mazuri kwa Watanzania wengi na kuongeza kwamba ipo mifano mingi, kama vile Kutuma na kupokea pesa kwa njia ya simu kwamba kumesaidia kuwapa huduma rasmi ya kifedha (akaunti ya fedha kwenye simu) watu wengi ambao awali haikuwezekana hadi uwe na akaunti benki.
Aliendelea kusema miaka ya nyuma kila malipo ya serikali au kutuma fedha ilibidi kwenda benki lakini sasa ivi unaweza fanya malipo au muamala sehemu yoyote ulipo na muda wowote kwa njia ya simu na kuongeza kuwa mtandao wa intaneti nao umebadili maisha ya wengi kwani umesaidia watu kuwasiliana vizuri zaidi na kwa gharama bora zaidi na hata kusaidia biashara kuanza na kukua.
Alizitaja faida za technolojia ya mawasiliano kuwa uwekezaji wake umesaidia kuinua maisha ya Watanzania. Huku sekta hii ikiendelea kupanuka, tayari imetoa ajira zaidi ya 1.5 milioni, zisizo za moja kwa moja kwenye maeneo kama wahandisi wa teknolojia, wasambaziji wa huduma na mawakala wa fedha.
Amesema ajira hizi zinasaidia mamilioni ya Watanzania kuwa na ajira na kipato cha uhakika na hivyo kuchangia kwenye uchumi wa nchi yao.Na kuongeza kuwa mchango wa sekta hii ni mkubwa na muhimu katika uchumi wa Tanzania.
Umuhimu wa sekta hii ya mawasiliano ya simu za mkononi unatukumbusha kuendelea kuunga mkono ukuaji wa sekta hii kisera, kimfumo na kimazingira ya uwekezaji. Hii itasaidia na kuhakikisha sekta hii inabaki imara, inakua zaidi na sote tunaendelea kunufaika na faida zake.