Serikali ya Tanzania yatoa maagizo Nida ili wananchi wapate namba

Muktasari:

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani,Masauni atembelea kituo cha kuchakata taarifa za waombaji wa vitambulisho  nchi nzima kilichopo Kibaha aagiza uongozi wa Nida kuongeza wafanyakazi na muda kutoka saa nane hadi 16 ili kuendana na kasi ya siku 20 zilizotolewa na Rais Magufuli.

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani nchini, Tanzania Hamad Masaun ameiagiza Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) kuongeza watumishi ili kwenda sambamba siku 20 za nyongeza zilizotolewa na Rais John Magufuli.

Desemba 27 mwaka 2019, akiwa wilayani Chato Mkoa wa Geita akisajili laini yake kwa alama za vidole, Rais Magufuli aliongeza siku 20 kuanzia Januari 1 hadi 20 mwaka 2020 akiwataka wasiosajili kufanya hivyo na  muda huo ukiisha hakuna kisingizio chochote kitakachokubalika huku akiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuzima laini zisizosajiliwa.

Masauni ametoa kauli  jana Alhamisi Januari 2, 2019 wakati alipotembelea kituo cha kuchakata taarifa za waombaji nchi nzima kilichopo Kibaha mkoani Pwani .

Naibu waziri huyo alimuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Nida, Dk Anold Kihaule kuongeza idadi ya watumishi katika kituo hicho pamoja na saa za kufanya kazi kutoka manane hadi 16 ili kuhakikisha wananchi wanapata namba na vitambulisho vyao ndani siku 20 zilizoongezwa.

“Nimetembea katika vituo mbalimbali vya Nida nchi nzima, changamoto kubwa wanayotoa wananchi ni kwenda kila siku kufuatilia kitambulisho au namba katika kituo husika. Lakini wamekua wakipata majibu kwamba bado kipo kwenye mchakato, wakati mwingine ameomba miaka mitatu iliyopita sasa anapoteza muda na gharama kufuatilia.”

“Nimekuja hapa leo (jana) nimegundua uchache wa watumishi, mkurugenzi ongeza watumishi hapa. Ongezeni muda sasa hivi wananchi wanafurika na kupata taabu vituoni huko, sisi ndiyo wawakilishi wao lazima tuwasemee na rais ameshatoa  maelekezo sasa ni utekelezaji tu,” alisema  Masauni.

Dk Kihaule alisema watayatekeleza maagizo hayo ya serikali huku akiwaasa wananchi waliopata namna za  utambulisho kwenda kusajili laini zao ili kwenda sambamba na muda ulioongezwa na Rais Magufuli.

 “Jumla ya watu milioni 7.6 tayari wana namba za utambulisho nchi nzima na kila siku tunaendelea kutoa namba hizo sehemu mbalimbali nchini,” alisema Dk Kihaule.