VIDEO: Serikali ya Tanzania yavifunga vyuo vyote kwa siku 30
Muktasari:
Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametangaza ongezeko la wagonjwa wawili wa virusi vya corona nchini humo mmoja amekutwa Zanzibar na mmoja Dar es Salaam wote ni raia wa kigeni hivyo kufikisha idadi ya watu watatu wenye corona.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imeagiza vyuo vyote vya elimu ya kati na juu vifungwe kwa muda wa siku 30 kuanzia leo Machi 18, 2020 ili kuondoa msongamano katika maeneo hayo na kuweza kujikinga na virusi vya corona (CODIV-19).
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema hadi leo Jumatano Machi 18, 2020, nchini kuna jumla ya watu watatu waliobainika kuwa na virusi vya corona ikiwa ni ongezeko la wagonjwa wawili.
Amesema mmoja ni raia wa Ujerumani (24) aliyegundulika Zanzibar na mwingine ni raia wa Marekani (61) aliyegundulika Dar es Salaam. Wote wapo katika uangalizi.
Waziri Mkuu amesema kwa sasa wanafunzi wengi wa vyuo wamefunga, hivyo amewataka wasirudi vyuoni hadi watakapotaarifiwa na walioko vyuoni wametakiwa warejee majumbani kwao ili kuondoa msongamano kwenye maeneo hayo.
“Vyuo vya ualimu wanafunzi wake walitakiwa kufanya mitihani Mei, waziri wa elimu, sayansi na teknolojia atafanya taratibu za kurekebisha ratiba ya mitihani kulingana na matokeo ya hali ya maambukizi,” amesema
Waziri Mkuu amewasisitiza wananchi waendelee na shughuli zao kwa umakini na wasiwe na taharuki kwani Serikali inaendelea kulifanyia tathmini suala hilo na kwamba itakuwa inatoa taarifa kadiri inavyohitajika.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema huduma katika maduka, masoko na za usafiri ziendelee kutolewa kama kawaida ila kwa umakini mkubwa na kwenye vyombo vya usafiri wa umma wahusika wahakikishe hawajazi sana abiria.
Jana, Machi 17, 20202 Serikali ilitanga kuzifunga shule zote za awali, msingi na sekondari kwa muda wa siku 30 na kwamba wanafuzi wa kidato cha sita waliopaswa kuanza mitihani Mei 4, 2020 nao watapaswa kusibiri Wizara ifanye utaratibu mwingine kulingana na matokeo ya hali ya maambukizi.
Waziri Mkuu alisema mikusanyiko yote mikubwa ya ndani na nje isiyo ya lazima imesitishwa kuanzia sasa ikiwemo shughuli za michezo, matamasha ya muziki, mikutano mbalimbali ikiwemo ya shughuli za kisiasa, mahafali na shughuli nyingine za kijamii.