Advertisement

Serikali ya Tanzania yawaonya viongozi wa dini wanaowapigia debe wanasiasa

Wednesday October 21 2020
serikalipic

Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania  imewakumbusha viongozi wa madhehebu ya dini kuacha kutumia majukwaa ya kisiasa kuwanadi wagombea wa vyama mbalimbali vya siasa kwani kufanya hivyo ni kuingilia uhuru wa kikatiba wa kila mtu kumchagua mgombea anayemtaka.

Mbali na kuingilia katiba, imeelezwa ni kinyume na kifungu cha 17 (c) cha Sheria ya Jumuiya sura ya 337 kama ilivyofanyiwa marekebisho na sheria namba 3 ya mwaka 2019 na kanuni zake  inayokataza viongozi wa dini kujihusisha na kitendo hicho.

Wito huo umetolewa leo Jumatano Oktoba 21, 2020 na Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene ambaye wizara yake ndio yenye wajibu wa kusajili na kusimamia jumuiya za kijamii na taasisi za dini.

Kauli hiyo imekuja katika kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28, 2020 ambapo baadhi ya viongozi wa dini wameonekana kuwanadi baadhi ya wagombea  wakieleza ndio wanaostahili kuchaguliwa kuliko wengine.

“Kumeibuka tabia ya baadhi ya viongozi wa dini na wanaojiita viongozi wa dini ambao wanatumia nyumba za ibada na majukwaa ya kisasa kueleza kuwa taasisi zao au makundi yao yanamuunga mkono au wanamuunga mkono mgombea fulani na wakimuahidi kumpigia kura mgombea huyo,” amesema Simbachawene.

Waziri huyo alieleza kuwa wizara yake inawakumbusha viongozi wa taasisi za dini kuepuka kutoa matamko ya kisiasa yenye lengo la kuhamasisha au yenye viashiria vya kuhamasisha na kuelekeza waumini wao kuchagua mgombea au chama fulani.

Advertisement

“Viongozi wengine wameonekana wakihamasisha na kutoa maelekezo kwa waumini wao kumchagua mgombea fulani. Vitendo hivyo ni kinyume na sheria.”

“Badala yake wazingatie sheria ya jumuiya ambayo inakataza viongozi wa dini kujihusisha na vitendo hivyo kwa kuwa vinaingilia uhuru wa kikatiba wa kila mtu kumchagua mgombea anayemtaka.”

Amesema wanatakiwa kuacha kutumia majukwaa na nyumba za ibada kuhamasisha na kuchochea waumini kumchagua au kutomchagua mgombea fulani.

“Viongozi watakaoshindwa kuzingatia masharti ya sheria za usajili wa jumuiya na katiba zao, wizara haitasita kuchukua hatua za kuifuta jumuiya hiyo au kutoisajili ambayo imewasilisha maombi yake,” amesema.

Advertisement