Serikali ya Tanzania yawaonya wanaokwamisha uwekezaji

Thursday September 12 2019Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa 

By Sharon Sauwa, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema itachukua hatua kwa watendaji wanaokwamisha mchakato wa wawekezaji nchini humo.

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameyasema hayo leo Alhamisi Septemba 12 2019 wakati akijibu maswali ya papo kwa hapo bungeni jijini Dodoma.

Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Jackline Msongozi ambaye amesema Serikali imeweka mkazo mkubwa katika kuboresha mazingira ya wawekezaji nchini lakini licha ya jitihada hizo kuna baadhi ya maofisa wanakwamisha

”Je, Serikali inatoa kauli gani kwa watendaji wa aina hiyo,” amehoji Msongozi.

Akijibu swali hilo, Majaliwa amesema Serikali kwa sasa imeweka utaratibu mzuri sana wa uwekezaji na wanaendelea kuhamasisha uwekezaji wa ndani na nje ya nchi Tanzania.

“Natambua kwamba tulipoanza kutoa wito wawekezaji kwa yeyote mwenye nia ya kuwekeza hapa nchini tulianza katika mapito mbalimbali watendaji wengine walikuwa hawajajua tunachokifanya,” amesema.

Advertisement

Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya tano imeweka utaratibu mzuri wa kuunda wizara ya uwekezaji ambayo sasa itashikilia sera ya uwekezaji kwa ujumla.

Amesema pia Serikali ina chombo kinachoshughulikia uwekezaji, Taasisi ya Uwekezaji  Tanzania (TIC) ambapo mambo yote yamewekwa ndani yake.

“Kwa utaratibu huu, kama bado kuna mtendaji anakwamisha uwekezaji huyo  atakuwa hana nia njema na nchi yetu na popote ambapo wananchi, waheshimiwa wabunge wanaona kuna mtendaji wa Serikali tumempa jukumu la kusimamia shughuli za Serikali ikiwemo la uwekezaji watoe taarifa,” amesema.

Amesema Serikali inatoa wito wa uwekezaji na imerahisisha uwekezaji kwa sababu kumekuwa na vikao na makundi mbalimbali vya wafanyabiashara wawekezaji hata Rais John Magufuli alikutana nao ili kujua kero zinazowakumba.

Amesema kwa sasa wametengeneza mfumo wa ‘Blue Print’ ambacho ni kitabu kinachoonyesha mabadiliko ya mifumo mbalimbali ya uwekezaji ambayo inarahisisha uwekezaji nchini ili uwe rahisi zaidi na ndio maana idadi imeongezeka.

”Tunaendelea kupokea kero za wawekezaji ili tuendelee kuboresha, naendelea kutoa wito kwa wawekezaji wote wasihofu kuja nchini, tuna ardhi, maliasili, tuna rasilimali za kuendeshea kilimo muhimu ni kufuata sheria na kanuni ndani ya nchi ili uweze kuwekeza,” amesema.

Advertisement