Shahidi kesi ya kina Mbowe adai polisi walimpiga risasi

Viongozi wa Chadema (waliokaa mtari wa mbele) wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kabla ya kuendelea kwa kesi ya uchochezi inayowakabili mahakamani hapo, jijini Dar es Salaam jana. Picha na Omar Fungo

Muktasari:

Aida Ulomi (50), shahidi wa upande wa utetezi katika kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi tisa wa Chadema ameieleza mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jinsi alivyopigwa risasi na polisi.

Dar es Salaam. Aida Ulomi (50), shahidi wa upande wa utetezi katika kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi tisa wa Chadema ameieleza mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jinsi alivyopigwa risasi na polisi.

Amesema alipigwa risasi akiwa anatoka nyumbani kwa mama yake mdogo eneo la Kinondoni, Dar es Salaam.

Shahidi huyo wa 12 ameeleza hayo leo Alhamisi Januari 23, 2020 wakati akitoa ushahidi katika kesi hiyo ya uchochezi. Viongozi hao akiwemo mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe wanakabiliwa na mashtaka 13.

Akiongozwa na Peter Kibatala ambaye ni wakili wa utetezi, Ulomi amedai alipigwa risasi mguuni na polisi aliodai kuwa walivamia kituo cha daladala cha Studio eneo la Kinondoni, karibu na jengo la ofisi za CCM.

Mbele ya hakimu mkazi mkuu wa mahakama hiyo, Thomas Simba, shahidi huyo wa 12 amedai jioni ya Februari 17, 2018 akiwa katika kituo hicho cha daladala akisubiri usafiri kwenda Kigamboni, aliona magari matatu ya polisi yakifika eneo hilo na askari walishuka na kuanza kufyatua risasi hewani.

“Nilikuwa nasubiri daladala nipande hadi Karume ili niunganishe magari ya Kigamboni ghafla niliona magari matatu ya polisi yaliyotokea Magomeni yakiwa na askari, haya magari huwa yanaitwa asante Makonda (Paul- mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam). Walipofika walishuka na kuanza kufyatua risasi hewani.”

“Watu waliokuwepo kituo cha daladala walisema ‘jamani hizi ni risasi za moto tukimbieni’, tukaanza kukimbia kuelekea katika lango la geti la ofisi za CCM,” amesema shahidi huyo.

Amesema kabla ya kuingia katika geti hilo alipigwa na kitu kizito mguuni na damu kuanza kutoka.

“Watu wengine waliendelea kukimbia kijana mmoja aniambia nimeshapigwa risasi, nilishindwa kutembea nikakaa chini, walikuja askari wanne wanaume wakasema sisi ndio tunafanya fujo,” amedai shahidi huyo.

Amesema baada ya muda walifika askari wawili wa kike na kumbeba kumpakia kwenye gari la polisi na kwamba askari wengine waliendelea kuwakamata watu wengine waliokimbilia katika jengo la CCM.

Amesema waliokamatwa walipelekwa katika kituo cha polisi ya Oysterbay.

Amebainisha kuwa baada ya kupigwa risasi hakupata matibabu hadi kesho yake saa nne asubuhi ndio akapelekwa hospitali ya polisi iliyopo Oysterbay.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni katibu mkuu wa Chadema, John Mnyika; naibu katibu mkuu- Zanzibar, Salum Mwalimu na Dk Vicent Mashinji.

Wengine ni mbunge wa Kawe, Halima Mdee; Ester Bulaya (Bunda), Esther Matiko (Tarime Mjini); John Heche (Tarime Vijijini) na Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini).

Kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji jinai kati ya Februari Mosi na 16, 2018,  jijini Dar es Salaam.