Sheikh Ponda kizimbani tena kuchuana na Serikali

Tuesday June 11 2019

 

By James Magai, Mwananchi

Dar es Salaam. Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda, leo Jumanne Juni 11, 2019 anapanda tena kizimbani katika Mahakama ya Rufani kuchuana na Serikali ya Tanzania wakati wa usikilizwaji wa rufaa inayomkabili.

Serikali ilikata rufaa inapinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyomfutia hatia Sheikh Ponda, baada ya kutengua hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam iliyomtia hatiani katika kesi ya jinai namba 245 ya 2012 iliyokuwa ikimkabili na wenzake 49.

Mahakama ya Kisutu katika hukumu yake iliyotolewa na Hakimu Mkazi Victoria Nongwa, Mei 9, 2013, ilimtia hatiani Sheikh Ponda peke yake kwa kosa la kuingia kijinai katika eneo la ardhi ya kampuni ya Agritanza Ltd, eneo la Chang’ombe Malkazi.

Licha ya kumtia hatiani Ponda, mahakama hiyo ilimwachia huru kwa masharti ya kutokutenda kosa lolote katika kipindi cha miezi 12 (mwaka mmoja), chini ya kifungu ncha 25 (g) cha Sheria ya Kanuni za Adhabu (Penal Code- PC).

Hata hivyo Sheikh Ponda kupitia kwa wakili wake Juma Nassoro alikata rufaa Mahakama Kuu akipinga adhabu hiyo na Mahakama Kuu katika hukumu yake iliyotolewa na Jaji Augustine Shangwa, Novemba 27, 2014, ilimfutia hatia hiyo Sheikh Ponda.

Nayo Serikali haikukubaliana na hukumu hiyo ya Mahakama Kuu ndipo ikakata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga hukumu hiyo.

Advertisement

Advertisement