Simulizi za kumbukumbu ya Nyerere zilivyosisimua kijijini kwake Butiama

Inaweza kuonekana ni hadithi ya kufurahisha kwa watu wengi, hasa wa maeneo ya mikoa inayolima mpunga na hivyo wali kuwa kati ya vyakula vyao vikuu.

Lakini katika maeneo mengi ambayo haizalishi zao hilo, miaka ya nyuma wali ulikuwa unaliwa katika matukio na vipindi maalumu, ikiwamo sherehe za machifu, harusi na misiba kwenye familia za watu wenye ukwasi.

Hiki ndicho kilichotokea kwa Jaji Joseph Warioba, wakati huo akiwa na umri wa miaka 12 alipokula wali kwa mara ya kwanza kwenye tukio maalumu nyumbani kwa Chifu wa Zanaki, Edward Wanzagi Nyerere.

Siku hiyo, Warioba pamoja na watoto na watu wengine kutoka eneo la Butiama iliyokuwa chini ya uongozi wa Chifu Wanzagi na Nyamswa kwa Chifu Makongoro Matutu waliitwa nyumbani kwa Chifu Wanzagi kumsikiliza Mwalimu Nyerere aliyerejea kutoka masomoni Chuo cha Makerere akiwa na harakati za kudai Uhuru wa Tanganyika.

“Siku hiyo tuliitwa nyumbani kwa Chifu (Chifu Edward Wanzagi Nyerere) ambapo Mwalimu Nyerere alipata fursa ya kuzungumza na vijana kuelezea nia ya kupigania Uhuru wa Tanganyika. Siku hiyo ndio nilipata fursa ya kwanza ya kukutana uso kwa uso na Mwalimu,” alisema Jaji Warioba, Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Serikali

“Nakumbuka ndiyo ilikuwa siku yangu ya kwanza kula wali. Nilikuwa na miaka 12,” anasema kwa kicheko ulioufanya umati uliohudhuria kongamano hilo pia kuangua kicheko

Ingawa hakutaja siku wala mwaka wa tukio hilo, kihesabu yawezekana Jaji Warioba aliyetimiza miaka 79 mwezi uliyopita alikula wali kwa mara ya kwanza mwaka 1952 ambayo ni miaka 12 tangu alipozaliwa mwaka 1940.

Jaji Warioba, Makamu wa kwanza Rais na Waziri Mkuu mstaafu ambaye wakati huo alikuwa kijana kutoka utawala wa Chifu Makongoro wa Ikizu, aliyekuwa rafiki mkubwa wa Chifu Wanzagi wa Zanaki amefichua siri hiyo Oktoba 14, mwaka huu wakati wa kongamano la kumbukizi ya miaka 20 ya kifo cha Mwalimu Julius Nyerere nyumbani kwake Mwitongo, Butiama.

Urafiki wa Chifu Wanzagi na mwenzake Makongoro ni chimbuko la urafiki wa kihistoria ya baba zao, Chifu Burito Nyerere wa Butiama na Matutu wa Ikizu.

Kongamano hilo lililopewa jina la “Nilivyomfahamu Nyerere” lililohudhuriwa na viongozi kadhaa wakiwemo wastaafu waliofanya kazi na Mwalimu Nyerere na viongozi wa sasa liliongozwa na Mkuu wa mkoa wa Mara, Adam Malima.

Msikilize Steven Wasira

Siyo Jaji Warioba pekee mwenye historia ya kufurahisha kuhusu jinsi alivyomfahamu na kukutana na Mwalimu Nyerere, bali hata mbunge wa zamani wa Bunda, Steven Wasira naye ana kumbukumbu ya kuvutia.

“Nilianza kusikia sifa za Mwalimu Nyerere nikiwa mtoto wa miaka 13; mwaka 1958 nilitoroka shuleni na kudandia lori kwenda eneo la Ikoma kumwona na kumsikiliza Nyerere baada ya kusikia ujio wake,” anakumbuka Wasira.

Kumbukumbu nyingine ya Wasira aliyejiunga na Umoja wa Vijana wa Tanu (Tanu youth league) akiwa na umri wa miaka 14 kabla ya kujiunga na kuwa mwanachama wa chama hicho mwaka 1959 ni jinsi Mwalimu Nyerere alivyomkasirikia kuhusu hoja yake ya kupinga makao makuu ya wilaya kuhamishwa kutoka Bunda kwenda Mugumu.

“Baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge mwaka 1970 nikiwa na umri wa miaka 25 na kuweka historia ya kuwa mbunge kijana kuliko wote, nilipiga kelele sana bungeni kupinga makao makuu kuhamishwa kutoka Bunda kwenda Mugumu. Baadaye nilienda Butiama kuzungumza na Mwalimu kuhusu hilo lakini hakunielewa,” anasimulia Wasira

Anasema kwa jinsi Mwalimu Nyerere alivyochukizwa hoja yake, kiongozi huyo alinyanyuka bila kumsemesha na kwenda shambani nyuma ya nyumba kupalilia ulezi.

Baada ya kupita muda mrefu bila Mwalimu Nyerere kurejea alipomwacha, Wasira anasema alilazimika kuwauliza walinzi aliko kiongozi huyo na kuambiwa yuko shambani anapalilia.

“Nilichukua jembe na kumfuata shambani; haiwezekani Rais wa nchi yuko shambani analima halafu mbunge nikae tu kumsubiri arejee tuzungumze. Tulilima kwa muda mrefu bila kusemezana. Nililima kwa nguvu na bidii na baada ya muda Mwalimu aliniita na kuniambia Mheshimiwa mbunge, yale yameisha; sasa tulime,” anasimulia Wasira

Mkongwe huyo wa siasa mchini anasema licha ya Mwalimu Nyerere kutokubaliana na hoja yake, baadaye kiongozi huyo alianzisha wilaya mpya ya Serengeti huku Mugumu ikiwa makao makuu na hivyo kuhitimisha suala la kuhamisha makao makuu kutoka Bunda.

“Mwalimu (Nyerere) alikuwa binadamu wa kawaida; alikasirika na hata kuadhibu; lakini alijaaliwa sifa na vipawa vingi vya ziada ikiwemo imani kuwa binadamu wote ni sawa, kusikiliza, kutafakari na kufanyia kazi hoja hata kama ni kinyume cha msimamo wake. Hili ni funzo kwetu kuwa tuchukie na kupinga hoja kwa hoja bila kumchukia mtoa hoja,” anasema Wasira.

Sifa za Nyerere kama za tembo kwa vipofu

“Ni vigumu kutaja na kuelezea sifa zote za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Kuelezea sifa za Nyerere ni sawa kundi la vipofu kuelezea sifa za tembo ambapo kila mmoja atamwelezea mnyama huyo kulingana na kiungo alichofanikiwa kugusa,”

Hiyo ni kauli ya Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mtumishi mstaafu wa umma, Mzee Sudi Ramadhani Simba (74) alipokuwa akizungumzia maadhimisho ya miaka 20 tangu kifo cha Mwalimu Nyerere.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Mwananchi jijini Mwanza, Simba, mtumishi mstaafu wa Shirika la Reli TRC anasema kueleza sifa zote za Mwalimu Nyerere ni vigumu kama ilivyo kwa kundi la vipofu kuelezea sifa za tembo baada ya kila mmoja kushika sehemu ya kiungo cha mnyama pori huyo mkubwa kuliko wote.

“Kwa maoni yangu, hakuna anayeweza kuelezea, kusimulia na kumaliza sifa zote za Mwalimu Nyerere kwa sababu ni nyingi, zimejaa na kuenea kila sehemu kuanzia vijijini, kata, wilaya na mkoa kwa jinsi alivyowagusa wahusika wa eneo hilo,” anasema Simba, Mwana CCM mwenye kadi namba B: 942178 aliyokata tawi la TRC jijini Dar es Salaam

Anataja baadhi ya sifa za Mwalimu Nyerere kuwa ni pamoja na kutokuwa ubaguzi wa aina yoyote, kipaji cha ushawishi, msimamo thabiti usiyoyumbishwa katika masuala ya msingi na upendo kwa wote.

Sifa zingine anazosema muasisi huyo wa Taifa alijaaliwa ni hekima, ujuzi wa kupanga maneno, muda sahihi wa kuzungumza na kujua hadhira inachohitaji kusikiliza au kuambiwa.

“Kipaji cha kujenga hoja, ushawishi na kupangilia maneno cha Mwalimu Nyerere kilijidhihirisha kwenye kikao cha Tanu kilichofanyika mjini Tabora mwaka 1958 na kupitisha uamuzi wa kura tatu,” anasimulia

Anasema wajumbe wengi wa kikao hicho wakiongozwa na watu maarufu waliokuwa na nguvu ndani ya Tanu walipinga hoja ya kura tatu ya kuchagua Mwafrika, Mhindi na Mzungu wakitaka wakitaka uchaguzi uwe wa kura moja pekee.

“Baada ya kuona msimamo wa wajumbe, Mwalimu Nyerere alikabidhi kwa muda nafasi ya uenyekiti kwa Mwalimu Kihere na yeye kuhamia upande wa wajumbe ili atetee msimamo wa kura tatu hadi akafanikiwa kushawishi wajumbe,” anasema.

Nyerere kushtaki kwa Mungu kulivyoliza umati

“Sitasahau kilichotokea katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Community Center mjini Tabora siku moja baada ya mkutano mkuu wa Tanu ulipitisha kura tatu baada ya hotuba na maneno ya Mwalimu Nyerere kuuliza umati uliohudhuria mkutano wa hadhara katika viwanja vya Community center mjini Tabora,” anasema

Simba ambaye ni mwanachama na shabiki kindakindaki wa timu ya Young Africans (Yanga) anakumbuka maneno yaliyoliza umati kuwa ni “Mwingereza akikataa kutupatia uhuru wetu tutamshtaki UNO (Umoja wa Mataifa) na UNO wasipotusikiliza tutashtaki kwa Mungu”

“Baada ya kutamka maneno hayo, Mwalimu Nyerere alilia machozi hadharani. Kitendo hicho (cha Nyerere kulia) kiliufanya umati wote, wake wanawake kwa wanaume pamoja na vijana kutoa kilio chenye kishindo kama sauti ya nyuki,” anakumbuka Simba na kufanya atokwe machozi katikati ya mahojiano

Baada ya kujifuta machozi na kunyamaza Simba anasema “kilichofuata baada ya kilio hicho ni kila mtu aliyekuwepo uwanjani hapo kuchomoa na kuonyesha juu silaha yake ya jadi aliyokuwa nayo kama ishara ya utayari wa mapambano dhidi ya mkoloni”

Anataja miongoni mwa silaha zilizoonyeshwa na waliohudhuria mkutano huo kuwa ni pamoja na visu, fimbo na bunduki za kienyeji maarufu kama korofindo.

“Hali ile (ya utayari) wa mapambano ilimshtua Mwalimu Nyerere kwa sababu alilenga kudai na kupata uhuru bila kumwaga damu,” anasema Simba

Anasema Mwalimu Nyerere alilazimika kutumia kipaji chake cha kujenga hoja na ushawishi kuwatuliza wananchi kudai uhuru kwa amani kwa badala ya mapambano ya silaha kwa sababu wakoloni walikuwa na jeshi na silaha bora zaidi yao.

Simba aliyegombea ubunge wa Tabora mjini kwa tiketi ya CCM kwa vipindi vitatu mfululizo bila mafanikio anasema matukio ya mkutano wa Tabora mwaka 1958 uliibua hamasa kwa vijana wengi kujiunga na chama hicho kudai uhuru.

“Wakati ule wanafunzi na watumishi wa umma hawakuruhusiwa kujihusisha na masuala ya siasa; tulikuwa tunatoroka shuleni kwenda ofisi za Tanu kufanya kazi za kujitolea kukijenga chama ikiwemo kuwachukulia kwa siri wazazi wetu kadi za chama,” anasimulia

“Ni wakati ule ndipo ilipoundwa TANU Youth League kuunganisha makundi mbalimbali ya vijana wapigania uhuru nchi nzima,” anaongeza