TPDC kutumia Sh1.3 trilioni kuchimba visima vya gesi

Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania  (TPDC),  Dk James Mataragio

Muktasari:

Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania  (TPDC),  Dk James Mataragio amesema watachimba visima viwili vya gesi katika kitalu cha Mnazi Bay Kaskazini kwa  Sh1.3 trilioni.

Mtwara. Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania  (TPDC),  Dk James Mataragio amesema watachimba visima viwili vya gesi katika kitalu cha Mnazi Bay Kaskazini kwa  Sh1.3 trilioni.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Novemba 2, 2019 Mataragio amesema, “kama tukigundua gesi, uendelezaji pamoja na uzalishaji itakwenda mpaka dola za kimarekani 450 milioni, hizo ni sawa na Sh1.1 trilioni ambazo tutaanza kuzitumia kwa muda, na sasa tuko katika hatua ya manunuzi i) na tutaendelea mpaka mwakani.”

Amesema gesi inayozalisha umeme kwa asilimia 60 inatoka Madimba na kwamba pamoja na kufanya utafiti na kusambaza gesi majumbani, viwandani na kwenye magari bado wanaendelea kuhamasisha watu kutumia nishati hiyo.

“Kiwanda cha Dangote tayari wanatumia gesi kuendesha mitambo yao,  wana mpango wa kutumia gesi kuendesha magari yao.”

“Niwapongeze  na niendelee kuwasihi wananchi kutumia gesi kwani ni nafuu ikilinganishwa na nishati nyingine, mfano ukitumia gesi nyumbani kuna punguzo la asilimia 40,” amesema  Mataragio.

Mkazi wa Mtwara, Salum Kaisi amesema mradi huo utasaidia kuvutia wawekezaji kwa kuwa kutakuwa na uhakika wa umeme.