VIDEO: Tamisemi yakiri uhaba walimu wa sayansi, yaomba kuajiri 15,000

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi, Mwita Waitara akijibu maswali ya wabunge wakati wa kipindi cha maswali na majibu bungeni jijini Dodoma leo. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

  • Licha ya kuajiri zaidi ya walimu 7,000 kwa masomo ya sayansi, bado kuna upungufu mkubwa wa walimu hususani masomo ya sayansi hivyo Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kuomba kibali cha kuajiri walimu 15,000.

Dodoma. Katika kipindi cha mwaka 2016/17 hadi 2018/19 Serikali ya Tanzania imeajiri watumishi 7,515 katika shule za sekondari nchini humo.

Kati ya watumishi hao, walimu walikuwa 7,218, fundi sanifu maabara 297 huku tatizo bado jambo ambalo limewafanya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kuomba kibali cha kuajiri walimu 15,000.

Akijibu swali bungeni leo Jumatano Septemba 11, 2019, Naibu Waziri wa Tamisemi, Mwita Waitara ameliambia Bunge la Tanzania kuwa kati ya walimu walioajiriwa, 29 walikuwa wenye mahitaji maalumu, 50 elimu maalumu wakati masomo ya sayansi na hisabati walikuwa 7,089 ambapo Lugha (literature in English) wamepangwa 100.

Naibu Waziri alikuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Anna Lupembe ambaye amehoji ni lini Serikali itapeleka walimu wa sayansi katika mko wa Katavi.

Waitara amesema katika kipindi hicho Mkoa wa Katavi ulipangiwa watumishi 121 katika shule za sekondari ambapo walimu wa masomo ya sayansi na hisabati ni 115 na fundi sanifu walikuwa sita.