Tanzania mwenyeji mkutano mawaziri wa maafa nchi za Sadc

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama Mpango Kabambe wa jiji la Dodoma baada ya kuuzindua kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, Februari 13, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Muktasari:

Tanzania itakuwa mwenyeji wa mkutano wa mawaziri wenye dhamana ya menejimenti ya maafa katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Kusini mwa Afrika (Sadc) utakaofanyika Zanzibar.

Dodoma. Tanzania itakuwa mwenyeji wa mkutano wa mawaziri wenye dhamana ya menejimenti ya maafa katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Kusini mwa Afrika (Sadc) utakaofanyika Zanzibar.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenister Mhagama  katika mkutano na waandishi wa habari leo Alhamisi Februari 13, 2020.

Amesema mkutano huo utafanyika Februari 18 hadi 21, 2020 na wengi wamethibitisha kushiriki.

Amesema katika mkutano huo, Tanzania inatarajia kujifunza mengi kutoka kwa mataifa yaliyopata maafa ingawa nao watapeleka uzoefu wao.

Amesema Comoro, Malawi, Msumbiji na Zimbabwe wamepitia katika maafa, watatoa uzoefu wao wa namna wanavyoweza kukabiliana na majanga.

"Tutajifunza mengi kupitia kwa wenzetu lakini kwetu itakuwa jambo la msingi kuwaambia namna tulivyojipanga,  si mnajua  tumepitia majanga pia," amesema.

Kwa mujibu wa Mhagama,  tetemeko la ardhi mkoani Kagera, kuzama kwa kivuko Ukerewe na ajali ya lori la mafuta mkoani Morogoro yatajadiliwa.