Tanzania yasema haijanyimwa mkopo na Benki ya Dunia

Msemaji wa Serikali ya Tanzania, Dk Hassan Abbasi

Muktasari:

Msemaji wa Serikali ya Tanzania, Dk Hassan Abbasi amewatoa hofu Watanzania kuhusu madai kuwa Benki ya Dunia (WB) imesitisha kutoa mkopo wa masharti nafuu wa Dola 500 milioni za Kimarekani kwa Tanzania, akibainisha kuwa bado wapo kwenye mazungumzo.

Dodoma. Msemaji wa Serikali ya Tanzania, Dk Hassan Abbasi amewatoa hofu Watanzania kuhusu madai kuwa Benki ya Dunia (WB) imesitisha kutoa mkopo wa masharti nafuu wa Dola 500 milioni za Kimarekani kwa Tanzania, akibainisha kuwa bado wapo kwenye mazungumzo.

Ameeleza hayo leo Alhamisi Januari 30, 2020 katika mkutano na waandishi wa habari mjini Dodoma.

Dk Abbasi ameeleza hayo baada ya kikao cha bodi ya utendaji ya Benki ya Dunia ambacho kingetoa uamuzi kuhusu kuruhusu mkopo huo kuripotiwa kuahirishwa.

Fedha za mkopo huo ambazo ni zaidi ya Sh1.2 Trilioni zingeelekezwa katika programu za shughuli za elimu.

Kikao hicho kilipangwa kufanyika Jumanne Januari 28, 2020  kwa ajili ya kuidhinisha mkopo huo, lakini kikaahirishwa dakika za mwisho kutokana na kile kilichoripotiwa na vyombo vya habari vya nje kuwa ni ombi la taasisi ya kijamii ambayo ina wanachama wake Tanzania.

Kabla ya kuahirishwa kwa kikao hicho, mkurugenzi anayehusika na haki za watoto wa taasisi ya kimataifa inayojishughulisha na haki za binadamu ya Human Rights Watch (HRW), Zama Neff aliiomba WB kuchelewesha fedha hizo hadi suala la wasichana wanaopata mimba shuleni litakapopatiwa ufumbuzi kuhusu mustakabali wa elimu yao.

Hadi Jumatatu Januari 27, 2020, nyaraka ya taarifa ya mradi huo wa Benki ya Dunia nakala yake ilionwa na The Citizen ilikuwa inaonyesha kuwa suala hilo lilikuwa halijatolewa uamuzi na Serikali kuhusu wanafunzi wa Tanzania  kurejea shuleni baada ya kuzaa. Pande hizo mbili zilikubaliana jinsi ya kusaidia wazazi hao kuendelea na shule.

Katika maelezo yake leo, Dk Abbasi amesema, “walipanga kukutana siku fulani, mmoja wa wawakilishi wao aliomba wakutane leo,  mtu anatoka hapo mishipa imekutoka eti mkopo umesitishwa, kukopa unaweza kuomba benki moja ukakosa nyingine ikakubali kwa hiyo ni majadiliano yanaendelea.”

“Huwezi  kwenda tu ukasema unakopa halafu ukakubaliwa lazima majadiliano yafanyike.”

Msemaji huyo wa Serikali alijibu madai ya mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe  kuwa Tanzania imenyimwa mkopo huo kwa madai kuwa fedha hizo zitatumika katika uchaguzi mkuu badala ya elimu.

“Tulifanya uchaguzi wa Serikali za mitaa, chaguzi za marudio na sasa tume za uchaguzi zinafanya vikao kwa ajili ya uchaguzi, sasa fedha hizo zinatoka Benki ya Dunia? Dunia haiwezi kuamini maeneo yake (Zitto). Dunia ina akili, ina macho” amesema Dk Abbasi.