Tanzania yataja sababu za kupungua kwa mauzo ya nje

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akizungumza bungeni alipokuwa akijibu baadhi ya hoja za wabunge waliochangia mjadala wa kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amesema ingawa mauzo ya nje ya nchi yanayotokana na sekta ya uvuvi Tanzania yalipungua mwaka 2018 lakini  hadi sasa mauzo hayo yamefikia dola za Marekani milioni 193, takwimu ambazo hazijawahi kutokea.

Dodoma. Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amesema kupungua kwa mauzo yanayotokana na sekta ya uvuvi nchini mwaka 2018 yanatokana na operesheni ya kuondoa uvuvi haramu.

Mpina ametoa kauli hiyo leo Jumanne Juni 25, 2019 wakati akijibu hoja zilizotolewa na wabunge waliochangia bajeti ya Serikali kwa mwaka 2019/2020 ya Sh33.1 trilioni.

Akijibu hoja ya kushuka kwa mapato yanayotokana na mauzo nje ya Tanzania, Mpina amesema takwimu zinaonyesha  katika sekta ya uvuvi mauzo kwa mwaka 2018 yalikuwa ni dola za Marekani milioni 158 lakini mwaka 2017 ilikuwa ni dola za Marekani milioni 193.

“Na miaka yote ile inacheza katika dola za Marekani 160. Lakini nawaambia wabunge tumefanya kazi kubwa mambo haya yametokana na operesheni za kuzuia uvuvi haramu wa mabomu,” amesema.

Mpina amesema hadi kufikia mwaka 2019 mauzo ya sekta hiyo yamefikia Dola za Marekani milioni 284 sawa na Sh654bilioni na kwamba haijawahi kutokea nchini.

Mwaka huu watakuwa wamenunua meli na kwenda kuvua bahari kuu na kwamba wamejipanga.

Aidha, amesema wabunge wamelalamikia tozo ya asilimia 0.4  inayotozwa bahari kuu na kwamba katika kutatua hilo kesho Jumatano wanakutana na waziri wa upande wa Zanzibar anayeshughulikia uvuvi ili waweze kujadili na kutoka na uamuzi.