Tigo inakusudia kuongeza watumiaji wa internet

Thursday October 31 2019

 

By Ephrahim Bahemu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Matumizi ya Internet hivi sasa yanaongezeka kwa kasi kubwa, kutokana na mtindo wa maisha watu wengi hujikuta wakifanya shughuli zao nyingi mtandaoni ziwe za kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Mpaka Juni 31, mwaka huu, watumiaji wa simu nchini Tanzania walikuwa milioni 43.75 huku kati yao asilimia 43 ambao ni sawa na watu milioni 23,14 wakitumia huduma za internet.

Kasi ya ongezeko la watumiaji wa internet imekuwa ni kama moto wa nyikani kwa sababu miaka sita iliyopita (2013) watumiaji wa huduma hiyo walikuwa milioni 9.3 tu.

Kutokana na mageuzi hayo, biashara nyingi zimehamia mtandaoni hata mitandao ya simu inakiri kuwa uuzaji wa data ni miongoni mwa vitu vinavyochangia mapato makubwa katika kampuni zao.

Kuhitaji internet ni jambo moja lakini kuwa na kifaa kinachokubali huduma hiyo ni jambo jingine, Ili kurahisisha mambo kampuni ya huduma za simu ya Tigo imeanza kuuza simu za vitufe (simu za tochi) lakini zenye uwezo wa internet ya 4G kama simu janja.

Simu hizo ambazo zimepewa jina la Kitochi 4G smart itakuwa ikiuzwa kiasi cha Sh49,000 na itakuwa na uwezo wa kuingia katika mitandao yote ya kijamii maarufu kama Whatsapp, facebook, twitter na Youtube.

Advertisement

Wakati akizindua simu hiyo Afisa Mkuu wa Biashara wa Tigo, Tarik Boudiaf alisema lengo ni kuhakikisha watu wengi zaidi wanaunganishwa na huduma ya Internet hususan 4G.

“Kwa muda mrefu gharama kubwa ya simu zenye uwezo wa 4G imekuwa kikwazo kwa Watanzania wengi kumiliki simu zenye uwezo wa intaneti ya kasi hivyo ujio wa simu hiyo ni msaada kwa watanzania wengi,” alisema Boudiaf.

Naye, Mkuu wa Bidhaa na Huduma wa Tigo, David Umoh alisema kwa hatua hiyo ana imani kuwa hakuna mtu ambaye atashindwa kupata manufaa yatokanayo na intaneti ya kasi ya 4G huku akifurahia mambo yote yanayopatikana katika smatifoni.

Advertisement