Treni ya abiria Dar es Salaam -Moshi kuanza safari Desemba 7

Tuesday December 3 2019

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Kuanzia Jumamosi Desemba 7, 2019 treni ya abiria kutoka Dar es Salaam kwenda Moshi itaanza kutoa huduma jambo litakalokuwa kicheko kwa abiria wa Kanda ya Kaskazini.

Treni hiyo imeshafanya majaribio mara kadhaa tayari kwa kuanza kutoa huduma ya usafiri utakaokuwa habari njema kwa abiria wengi, hasa kipindi hiki cha kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka.

Akizungumza jana Jumatatu Desemba 2, 2019 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,  Isack Kamwelwe amesema jena treni hiyo ilikwenda Moshi ikitokea Dar es Salaam  ikiwa na wafanyakazi wa Shirika la Reli (TRC) na baadhi ya  wataalam wa usafiri waliojiridhisha ipo vizuri kuanza kubeba abiria.

“Naomba Watanzania waelewe kwamba treni ya Dar es Salaam kwenda Moshi tayari tumeijaribu na kila ilipopita wananchi walikuwa wanaishangilia hii ni kuonyesha namna gani walikuwa wakiisubiri.”

“Hivyo  itaanza kufanya kazi rasmi Desemba 7 mwaka huu, wakae mkao wa kula kwani ipo tayari kwa kubeba abiria,” amesema Kamwelwe.

TRL imetangaza nauli ya treni hiyo itakayopita Korogwe mkoani Tanga; Dar es Salaam hadi Korogwe daraja la tatu itakuwa Sh10,700, daraja la pili kukaa Sh15,300 na daraja la pili kulala Sh25,400.

Advertisement

Kutoka Dar es Salaam kwenda Moshi daraja la tatu ni Sh16,500, daraja la pili kukaa Sh23,500 na daraja la pili kulala Sh39,100.

Advertisement