Ubunge unavyowagombanisha Waitara, mwenyekiti CCM Mara

Muktasari:

  • Uchaguzi wa madiwani, wabunge wa Rais nchini Tanzania unafanyika mwaka 2020 ambapo tayari baadhi ya wagombea wameanza kujitokeza kutangaza nia za kuwania nafasi hizo huku zikiibua mvutano ndani ya vyama vyao.

Serengeti. Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi) nchini Tanzania, Mwita Waitara ameweka wazi msimamo wake wa kuwania ubunge Tarime Vijiji huku akidai haogopi kuitwa kwenye kamati ya maadili ya CCM kwa kuwa hajavunja kanuni.

Januari 1, 2020 Waitara aliweka wazi msimamo wake huo na kuibua mjadala ikiwamo tamko la Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Samwel Kiboye maarufu namba Tatu, aliyetoa onyo watamchukulia hatua kwa kujitangaza kinyume na kanuni na taratibu za chama.

Kiboye alisema, “Tarime sasa hivi inatuumiza sana vichwa, mtu anajitangaza kuwa atajitokeza kugombea, anatumia kanuni gani? anagombeaje ni nani amempitisha kugombea? huku atatuletea makundi na tayari ameishatuletea.”

Alisema wana kanuni, katiba na vikao ndivyo vinapitisha mgombea.

Alikwenda mbali zaidi na kudai wanatumia majina ya viongozi wakubwa kuwa wamewatuma.

Alipoulizwa na Mwananchi kwa simu kuhusu uamuzi huo wa kujitangaza kugombea kinyume na kanuni, Waitara alihoji iwapo mwenyekiti huyo hajui utaratibu wa kupata wagombea au la.

“Tena umefanya vizuri kunitafuta nami nieleze nilichodhamiria, najua ninachokifanya, narudia tena nitawania nafasi Tarime vijijini,” alisema Waitara kwa msisitizo

Alisema alishangaa kuona taarifa kwenye mitandao Mwenyekiti akichachamaa.

“Anadai ataniita kwenye kikao cha maadili cha chama, niko tayari maana hapo ndipo uamuzi sahihi utatokea, maana mengine hayana maana, mawazo ya Kiboye si chama maana hayo si maazimio ya chama aliyotoa kwenye mitandao.”

Alisema hajui kosa lake ni lipi kutangaza nia yake kwenye jimbo linaloongozwa na wapinzani huku akihoji pia kwamba mwenyekiti huyo hajasema kanuni aliyoivunja.

Jimbo hilo la Tarime Vijijini kwa sasa linaongozwa na John Heche wa Chadema.

Waitara alifafanua yeye ni kiongozi akiwa mwenyekiti alipaswa kumuita na kumweleza si kutoa taarifa ambazo zimeibua hisia kubwa kwa jamii.

Kuhusu jimbo lake la Ukonga jijini Dar es Salaam alisema kupitia taarifa yake ya kutia nia Tarime vijijini ni wazi hatagombea huko na kuwa amefanya hivyo ili watu wengine wenye nia wajitokeze.

Waitara mwaka 2015 alichaguliwa kuwa mbunge wa Ukonga akiwa Chadema lakini mwaka 2018 alitangaza kujiuzulu na kuhamia CCM ambako alipitishwa tena kugombea jimbo hilo na kushinda.

Alipotafutwa Kiboye ili kutaka kujua  kama wameishamwita Waitara na kama bado lini wanatarajia kufanya hivyo, alijibu kwa kifupi, “mwandishi hilo ni siri siwezi kulisema sasa na msimamo nishautoa.”