Uchaguzi Bavicha ni mshikemshike, wagombea watoa neno

Monday December 9 2019

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) leo Jumatatu Desemba 9, 2019 linafanya uchaguzi wa viongozi wake.

Watakaochaguliwa leo baada ya kupigiwa kura na wajumbe 371 wa mkutano huo wa baraza hilo unaofanyika katika ukumbi wa Mlimani City ni mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa bara na Zanzibar.

Viongozi watakaopatikana leo  wataliongoza baraza hilo kwa kipindi cha miaka mitano.

Wanaowania uwenyekiti ni  John Pambalu, Dorcas Francis na Mathayo Gekul ambao wamezungumza na Mwananchi na kila mmoja kueleza atakachokifanya ikiwa atachaguliwa.

Uchaguzi  wa mwenyekiti wa Bavicha mwaka 2014 walipitishwa wagombea 13 na Partobas Katambi kuibuka mshindi baada ya uchaguzi kurudiwa mara mbili.

Safari ya pili Katambi aliyehamia CCM Novemba 21, 2017 na baadaye kuteuliwa kuwa mkuu wa wilaya ya Dodoma mjini, alichuana na Upendo Peneza ambaye ni mbunge wa viti maalum Chadema.

Advertisement

Baada ya Katambi kuhama Chadema, nafasi yake ilichukuliwa na Patrick Ole Sosopi ambaye alikuwa makamu mwenyekiti bara wa baraza hilo.

Pambalu ambaye ni mwalimu kitaalama amesema, “nikishinda, nitakwenda kujenga sura ya kitaasisi ya Bavicha na ya kiharakati kwani imekosekana kwa sasa.”

“Nia na dhamira ya kushinda ninayo na ikiwa hivyo nitakwenda kuyafanya haya kwani uwezo huo ninao ambao nimeutumia na naendelea kuutumia nikiwa diwani wa Butimba Mwanza na makamu mwenyekiti bara,” amesema Pambalu ambaye ana shahada ya ualimu.

 Dorcas amesema Bavicha ni taasisi sio ya mtu mmoja, “kwa kuwa vijana ni nguvu kazi ya mabadiliko, nitakwenda kuwatumia ili kuhakikisha tuna baraza  imara lenye chachu ya mabadiliko.”

Msomi huyo mwenye shahada ya mahusiano ya umma amesema, “najiamini nitashinda, kwanza ni mwanamke pekee, unapokwenda vitani lazima uwe na uhakika wa kushinda lakini kama sitashinda hakuna tatizo, mapambano yataendelea.”

Gekul amesema, “baraza la vijana kwa hali ya kisiasa ilivyo linahitaji kuwa na kijana jasiri na anayejiamini vya kutosha na hizi sifa ninazo na nitakwenda kushinda kwa kishindo.”

Gekul mwenye shahada ya ugavi amesema akifanikiwa kushinda kuwa mwenyekiti, “nitakwenda kutoa elimu ya kutosha kwa vijana ili kutambua wajibu wao.

Akijibu swali iwapo akishindwa itakuwaje, Gekul ambaye ni diwani wa Ari, Babati mkoani Manyara amesema, “nakwenda kushinda hapa nimekuja tu kuthibitishwa lakini kama sitashinda ifahamike sijaja Chadema kuwa mwenyekiti wa Bavicha lakini nina imani katika ukombozi wa Taifa hili utaletwa na Chadema.”

Endelea kufuatilia Mwananchi kupata habari zaidi kuhusu uchaguzi huo

Advertisement