Ukimya wa wazazi unavyowatesa vijana walioambukizwa VVU utotoni

“Kati ya mitihani migumu ninayopitia ni namna nitakavyomwambia mwanangu ukweli kwamba nilimuambukiza VVU alipokuwa anazaliwa. Sijui siku hiyo itakuwaje, nawaza sana,”

Huyu ni mama wa mtoto anayesoma darasa la saba katika shule moja jijini Dar es Salaam, Happines Gaisan (sio jina halisi) akizungumzia ugumu anaopata kumweleza mwanae juu ya afya yake.

Happiness alifunguka kinachomsibu wakati shirika la kimataifa linalohudumia na kutoa msaada wa kisaikolojia kwa watoto la Psychosocial Wellbeing For All Children (Reppsi) lilipoadhimisha siku ya Ukimwi duniani kwa kuandaa mjadala wa vijana na maambukizi mapya ya VVU.

Mtoto wa Happiness mwenye umri wa miaka 14 anatumia dawa za kufubaza VVU (ARVs), lakini hajui kwanini anatumia dawa hizo.

“Anachojua yeye ni kwamba asipokunywa ngozi yake itaharibika na kupata vidonda, huwa namsimamia na kila siku anakunywa,” anasema Happiness ambaye pia anaishi na VVU kwa miaka 16 sasa.

Kinachomtesa Happiness ni hofu kwamba mwanae atapokeaje majibu.

“Hata hivyo najipanga siku yoyote nitamweleza kwa sababu tayari amekua, atanielewa,” anasema Happiness.

Reppsi ilianzisha mradi wa Ready Plus baada ya kubaini vijana wengi wapo gizani na wanapojua kuhusu afya zao bila msaada kisaikolojia, hukata tamaa kimaisha kwa kudhani ndoto zao zimekufa.

Mkurugenzi mkazi wa Reppsi, Edwick Mapalala anasema ukweli ni kwamba wazazi wengi wapo ‘bubu’, sio Happines peke yake.

Wengi hawathubutu kuwaambia ukweli watoto wao kuhusu afya zao wakihofia itakuwaje na badala yake wanawaacha watoto wenyewe wagundue.

Anasema kukaa kimya ni hatari kwa makuzi ya watoto kwa sababu ni rahisi kwao kuambukiza wengine au kujidhuru pale watakapojua.

“Tunachofanya ni kuwasaidia vijana kutambua afya zao, kujikubali ikiwa watabainika na VVU, kuwa wafuasi wazuri wa dawa na wasio na VVU kujitunza,” anasema Mapalala.

Maadhimisho ya wiki ya Ukimwi duniani kwa mwaka huu 2019 yamefanyika mkoani Mwanza huku ujumbe ukielekezwa kwa jamii kushiriki kikamilifu katika vita dhidi ya Ukimwi. Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Tume ya kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) ndiyo iliyoratibu maadhimisho hayo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Kazi na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama anasema takwimu zinaonyesha kundi la vijana wa umri wa miaka 15 hadi 24 linachangia maambukizi mapya ya VVU kwa asilimia 40.

Mhagama anasema hali hiyo inalifanya kundi hilo kuwa kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata maambukizi ya VVU kuliko kundi lingine.

“Kauli mbiu hii inatilia mkazo kwenye kuunganisha nguvu katika kupunguza maambukizi mapya ya VVU na hasa kwenye kundi la vijana,” anasema.

Hata hivyo, mkakati mkubwa wa Serikali ni kufikisha asilimia tisini tatu ya kwanza ikiwa kupima na kubaini afya, ya pili walio na maambukizi kuanza dawa na wanaotumia dawa kuwa wafuasi wazuri.

Simulizi za vijana

Neema Khalid (20), anasema alijua kuhusu afya yake akiwa kidato cha pili.

“Mama yangu hakuwahi kuniambia ukweli kama naishi na VVU, kila siku nilikuwa nabadilishiwa magonjwa, mara kichwa, sikoseli siku nyingine naambiwa tumbo, nilikuwa naamini,” anasema Neema.

Anasema siku moja alichoka kutumia dawa na kwa sababu manesi walikuwa na lugha wanayotumia wakati akichukua dawa alitaka kujua uhalisia wa ugonjwa wake.

“Kuna wakati walikuwa wananiambia hizi ni dawa kwa ajili ya mdudu, nikawa najiuliza mdudu gani? Ndio siku hiyo nikaelezwa ukweli,” anasema Neema ambaye hahofii jina lake halisi kutumika.

Anasema alichanganyikiwa, hakuamini kile alichoambiwa na kwa wakati ule alikata tamaa ya maisha kabisa.

Anasema kwa sababu alijua ukweli wakati akijiandaa kufanya mitihani ya kidato cha pili hakufanya vizuri mitihani hiyo.

“Nilikuwa nakuwa kwenye kumi bora katika mitihani, lakini baada ya kujijua ufaulu wangu ulishuka sana. Nilikuwa wa zaidi ya 20,” anasema Neema.

Anasema aliumia sana kwa nini mama yake hakumwambia mapema kuhusu hali yake.

“Vijana wanaweza kuwa wanafanya ngono, sasa kama hujijui si unaweza kumuambukiza mwingine? Hii ndiyo hatari kubwa ninaoogopa,” anasema Neema.

Wakati akiwa kwenye maumivu hayo alikutana na Reppsi ambao walimpatia mafunzo ya kujitambua, kujikubali, kuona maisha lazima yaendelee na kutakiwa kuwafundisha vijana wenzake.

“Mpaka leo nafanya kazi ya kuwasaidia wenzangu na wengi kusema kweli wanakunywa dawa hawajijui. Huwa nakuwa hospitali ya Palestina, Sinza na kupitia kwangu, vijana wengi wamejitambua,” anasema Neema.

Kijana mwingine, Twaha Selemani ambaye pia yupo huru kutumia jina lake halisi anasema siku alipobaini kuhusu afya yake alichanganyikiwa.

Naye hakuwahi kuambiwa kuhusu afya yake mpaka alipoamua mwenyewe kutafuta ukweli.

“Nakumbuka ilikuwa mwaka 2009 nilipojua, sikujikubali kabisa, sikuamini kama naishi na VVU japo nilipopima niliambia naishi navyo,” anasema Twaha.

Anasema wakati alipotakiwa kutumia dawa za ARVs hakuwa mfuasi mzuri kwa sababu akili yake haikukubali jambo aliloambiwa.

“Kuna wakati nilipewa dawa nikawa natupa sinywi kwa sababu zilinichefua na mimi sikuwa na uhakika kama naishi na VVU, hali ikawa mbaya zaidi,” anasema.

Kijana huyo alianza kujikubali baada ya kupewa msaada wa kisaikolojia na baadaye kuwekwa kwenye kundi la kuwaelimisha wenzake kuhusu VVU.

Twalib Abdul, anasema kama ilivyo kwa wenzake wengi naye hakuwahi kuambiwa afya yake mapema.

“Nilijua wakati nipo sekondari, hakuna kazi ngumu kama kupokea majibu kwamba unaishi na VVU, niliumia sana kusema kweli wala sikuamini,” anasema kijana huyo.

Anasema ingawa alikata tamaa aliendelea kufuatilia taarifa za ugojwa huo ndipo alipobaini kwamba sio peke yake, vijana wenzake wengi hawajijui. “Nikaamua kuwasaidia, huwa nashinda kwenye vituo vya afya nikiwaona vijana nawafuatilia na nikijua wanahitaji kujijua, nawashauri wafanye hivyo,” anasema Twalib.

Ujumbe wao kuhusu Ukimwi

Vijana hao wanatamani kuona watoto wanatambua afya zao mapema ili waendelee kuwa wafuasi wazuri wa dawa za ARVs.

“Unaweza kufubaza VVU ukawa na sifuri kabisa na utafanya hivyo ukishajijua. Kama hujijui huwezi kutilia maanani jambo hilo,” anasema Twalib.

Neema anawaomba wazazi wavunje ukimya kwa sababu ni muhimu kuwaeleza ukweli watoto wao pale anapobaini kuwa wamepevuka na wanaweza kuelewa kuhusu hali zao.

“Wazazi wawe wawazi kwa watoto, mtoto akijua afya yake atajitunza na asipojua anaweza kuambukiza wengine, jambo ambalo sio sawa,” anasema.

Anasema madhara mengine ya kutojua afya mapema kwa watoto waliozaliwa na VVU ni kujiua pale wanapobaini, kukata tamaa, kufeli masomo na kujinyanyapaa wao wenyewe.

Mbali na kuambukiza wengine, wasipojua kuhusu afya zao wanaweza kuacha matumizi ya dawa, jambo ambalo pia ni hatari kwa afya zao.

“Kuishi na VVU sio mwisho wa maisha. Ukimwi sio kifo,” hivi ndivyo anavyosema Twalib na kuongeza:

“Unaweza kuishi miaka mingi ikiwa baada ya kupima na kuitambua afya yako utaanza matumizi sahihi ya dawa za kufubaza virusi vya ugonjwa huo”.

Neema naye anasema: “Ukiambiwa unaishi na VVU haimaanishi utakufa, unaweza kuolewa, kuoa, kuzaa na kuishi maisha marefu ikiwa utakuwa mfuasi mzuri wa dawa.”

Unyanyapaa

Mapalala anasema ukimya wa wazazi unatokana na tatizo la unyanyapaa kwenye jamii.

“Wazazi wanahofia wakiwaambia watoto watajinyanyapaa au watachukua hatua mbaya zaidi, kwa hiyo wanakaa kimya mpaka wakati mwingine mtoto wanafikisha miaka zaidi ya miaka 18,” anasema Mapalala.

Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Shirika la Pasada la Roman Katoliki Jimbo la Dar es Salaam, Ester Mbwana anasema wazazi wanapaswa kuvunja ukimya.

“Sisi tunajitahidi kuwafikia vijana na kuwasaidia kuhusu Ukimwi, hata hivyo bado jamii inatakiwa kushirikiana kwa pamoja tunaweza kuifanya Tanzania kuwa sifuri kwenye maambukizi,” anasema Mbwana.