VIDEO: Chama cha saba chajitoa, CCM yatamba

Thursday November 14 2019

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu mchakato wa ushiriki wa chama hicho kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa. Picha na Ericky Boniphace 

By Bakari Kiango na Nazael Mkiramweni, Mwananchi [email protected]

Dar/mikoani. Wimbi la vyama vya siasa kususia uchaguzi wa serikali za mitaa limeendelea baada ya chama cha NLD nacho kuungana na vyama vingine sita.

Wakati vyama hivyo vikitangaza uamuzi huo, CCM imesema itaendesha kampeni safi katika uchaguzi huo wa Novemba 24.

Vyama ambavyo vimetangaza kwa nyakati tofauti kutoshiriki uchaguzi huo ni Chadema, ACT- Wazalendo, UPDP, CUF, Chauma na NCCR-Mageuzi.

Vyama hivyo vimejitoa vikidai kutotendewa haki kwa wagombea wao kunyimwa fursa ya kuchukua fomu za kugombea katika ofisi za watendaji au kushindwa kuzirejesha kutokana na ofisi hizo kutofunguliwa au kufunguliwa lakini mtendaji anakuwa hayupo.

Taarifa iliyotolewa jana na Mwenyekiti wa NLD, Oscar Makaidi ilisema hawatashiriki uchaguzi huo kutokana na ukiukwaji wa makusudi wa taratibu, kanuni na sheria ya uchaguzi.

“Tumepokea malalamiko mbalimbali kutoka kwa wagombea wetu yanayothibitisha ukiukwaji na ubakwaji wa demokrasia nchini kwa kiwango cha kutisha kiasi cha kufanya uchaguzi huu kuwa kituko. Kwa ujumla uchaguzi umepoteza sifa ya kuitwa uchaguzi,” alisema Makaidi.

Advertisement

Mwenyekiti huyo alisema “nawaomba wanachama na wagombea wote nchi nzima kuwa watulivu na kutojihusisha kwa lolote kuhusiana na uchaguzi huu mpaka hapo tutakapowataarifu vinginevyo.”

Kutokana na kadhia hiyo, wadau waliozungumza na Mwananchi juzi walisema meza ya mazungumzo ya pamoja na kuundwa kwa chombo huru cha kusimamia kazi hiyo ndiyo suluhisho la changamoto hizo.

Tayari Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo ameshatoa kauli nne katika muda wa takriban wiki moja, akijaribu kurekebisha, kufafanua na kuelekeza wasimamizi wa uchaguzi, jambo ambalo limekosolewa na wapinzani wakihoji madaraka yake kisheria.

Wakati vyama hivyo saba vikijitoa, vyama 11 visivyo na wabunge vimeahidi kushiriki uchaguzi huo. Vyama hivyo ni DP, NRA, AFP, Demokrasia Makini, UDP, Ada-Tadea, Sauti ya Umma (Sau), TLP, CCK na UMB.

Kwa upande mwingine, msimamizi wa uchaguzi wa Chadema katika Mkoa wa Dodoma, Benson Kigaila akizungumza na wanahabari jana alisema baada ya kujitoa katika uchaguzi huo sasa wanaanza kutafuta majibu ya changamoto hizo kupitia wananchi na vikao vya chama na uchaguzi mkuu ujao hawatajitoa.

“Chama cha siasa kazi yake kubwa ni kuchukua madaraka ya dola ili kutumia sera, falsafa na itikadi yake kuleta mabadiliko ambayo kinaona yanafaa, lakini kuanzia sasa hadi mwaka 2020 wawe wanapenda au hawapendi lazima tutafute majibu kwa kupitia Watanzania pamoja na kupitia vikao vya chama,” alisema.

Hata hivyo hali ni tofauti kwa chama tawala ambacho kimeendelea kutamba kufanya vizuri.

Katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amesema wamejipanga kufanya kampeni za kistaarabu.

“Hii ni siri, lakini leo nataka niwaambie siri ya mkakati wa chama kuelekea uchaguzi huu. Tutakuwa na watu milioni 1.3 watakaosimamia uchaguzi huu kuanzia ngazi ya shina hadi mkoa.”

Katibu huyo wa uenezi, alitumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali kwa kutoyumbishwa na msimamo wa baadhi ya vyama vya upinzani vilivyojitoa katika mchakato huo akisema vilishindwa kufuata utaratibu na kanuni za uchaguzi.

Advertisement