VIDEO: Dk Mwinyi aapishwa urais Zanzibar

VIDEO: Dk Mwinyi aapishwa urais Zanzibar

Muktasari:

  • Dk Hussein Mwinyi ambaye amewahi kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), ameapishwa leo Jumatatu Novemba 2, 2020 kuwa Rais wa nane wa Zanzibar baada ya Dk Mohammed Shein kumaliza muda wake

Dar es Salaam. Rais mteule wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ameapishwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa awamu ya nane.

Mwinyi amekula kiapo hicho leo Jumatatu Novemba 2 katika uwanja wa Amani mjini Unguja, ambako sherehe za kuapishwa kwake zimefanyika na kuhitimishwa.

“Mimi Hussein Ali Mwinyi, naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu kwamba nitakuwa mwaminifu kwa Zanzibar na kuitumikia kwa moyo wangu wote na kwamba, nitaihifadhi, nitailinda, nitaitii na kuitetea Katiba ya Zanzibar na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na watu wake kwa mujibu wa sheria iliyowekwa,” ndivyo alivyoapa kiongozi huyo.

Baada ya kuapa, Rais Mwinyi alipokea dua kutoka kwa viongozi mbalimbali wa dini ambao walimuombea heri katika uongozi wake wa miaka mitano baada ya kuchaguliwa katika uchaguzi wa Oktoba 27 na 28.

Kiongozi huyo alitoka kwenye jukwaa la kiapo na kuelekea kwenye jukwaa la saluti ambapo vikosi vya jeshi vilitengeneza umbo la Alfa kama ishara ya mwanzo wa utawala wake baada ya Rais Ali Mohamed Shein kumaliza muda wake.

Rais Mwinyi alipokea heshima kwa kupigiwa mizinga 21 wakati wimbo wa Taifa ukipigwa na baada ya hapo alikwenda kukagua gwaride hilo likiwa katika umbo la Alfa, kisha kuelekea katika jukwaa kuu ambalo waliketi viongozi mbalimbali wakishuhudia kiapo hicho.

 Alisalimiana na viongozi mbalimbali waliokaa kwenye jukwaa kuu wakiwamo marais wastaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na Dk Shein sambamba na marais wastaafu wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi ambaye ndiyo baba yake mzazi na Jakaya Kikwete Rais wa Awamu ya Nne wa Muungano.

Vikosi vya jeshi vilitoa kiapo cha utii kwa Rais mpya na kuimba wimbo wa Taifa la Zanzibar ambao uliimbwa na askari wote pamoja na wananchi waliokuwa wakishuhudia gwaride hilo maalumu.

Baada ya wimbo huo, askari wa vikosi maalumu vya JWTZ walifanya maonyesho mbalimbali wakipita mbele ya Rais mpya kama ishara ya uimara wao katika kuilinda nchi yao.

Ndege za kivita nazo zilipita juu ya uwanja huo kutoa heshima kwa Rais mteule na kushangiliwa na wananchi waliokuwa wakishuhudia kitendo hicho kwa furaha.