VIDEO: Hali ngumu zaidi sakata la Tito Magoti

Dar es Salaam. Sakata la kushikiliwa kwa mfanyakazi wa kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Tito Magoti linazidi kuwa gumu baada ya kufikishwa mahakamani, huku polisi Kinondoni ikikana ofisa huyo kukamatwa wilayani humo.

Magoti alichukuliwa Ijumaa iliyopita na watu wasiojulikana waliovalia kiraia akiwa eneo la Mwenge. Siku hiyo jioni Kamanda wa Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alitoa taarifa kuwa wanamshikilia ofisa huyo na wenzake watatu.

Hata hivyo, hakueleza yupo kituo gani lakini akasema Magoti (26) amekamatwa kwa tuhuma za jinai ambazo hakuzibainisha, hali iliyosababisha hofu kwa familia pamoja na wafanyakazi wenzake.

Licha ya jitihada za mkurugenzi mtendaji wa LHRC, Anna Henga na watendaji wake kuzunguka vituoni pamoja na kituo kikuu kumtafuta, bado hawajaweza kufanikiwa.

Hilo lilisababisha Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadami (THDRC) na Mtandao wa Wanawake Watetezi wa Haki za Binadamu (WHRDs) wamefungua kesi Mahakama Kuu kumshitaki Mambosasa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kutaka walazimishwe kumpa dhamana.

Moja ya mambo yanayotia ugumu suala hilo ni kutofautiana kwa kauli za makamanda wa polisi.

Wakati Mambosasa akieleza kuwa Magoti alikamatwa eneo la Mwenge, kamanda wa polisi wa Kinondoni, Musa Taibu aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa hana taarifa ya kukamatwa kwa ofisa huyo “katika himaya yake”.

Kamanda Taibu alitoa kauli hiyo katika mkutano wake na waandishi wa habari alipokuwa akitoa tahadhari kwa wananchi wa Kinondoni kusherehekea sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya bila kuvunja sheria. “Kwa bahati mbaya sina taarifa hizi,” alisema Taibu.

“Nimeuliza wenzangu hakuna mwenye taarifa za kukamatwa kwa Tito kwenye kwenye himaya yangu. Inawezekana amekamatwa kwa siri na mtu mwingine asijue kwa ajili ya kufanikisha jambo fulani. Na si kila jambo linalofanyika lazima polisi ijue. Inategemea jambo linalozungumziwa ni la aina gani na lina usiri kiasi gani.”

Mashuhuda walioongea na vyombo vya habari walisema Magoti alikamatwa akiwa eneo la kituo cha mafuta Mwenge, umbali usiozidi nusu kilomita kutoka kituo kidogo cha polisi cha Mwenge wilayani Kinondoni.

Lakini jana saa 12:24 jioni, Mwananchi ilimtafuta Kamanda Mambosasa ambaye alisema “suala hilo limeshatolewa ufafanuzi na makao makuu”.

Alipoulizwa alipo Magoti na wenzake, Mambosasa alisema “ametunzwa na kanda”, lakini akasema maelezo zaidi atafutwe mkurugenzi wa upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz.

Mwananchi ilipomuuliza kuhusu kauli ya Kamanda Taibu kuwa hafahamu lolote kuhusu kukamatwa kwa ofisa huyo wa LHRC, Mambosasa alisema: “Huyu wa Kinondoni anachanganya mambo, ana shida huyo. Kwanza si msemaji wa polisi. Alichokisema ni maoni yake.”

Jitihada za kupata ofisi za makao makuu kuzungumzia suala hilo hazikufanikiwa.

Jana, katika hali inayolitia ugumu zaidi suala hilo, mwanasheria wa THDRC, Onesmo Ole Ngurumwa alisema wamefungua shauri hilo Jumapili kwa njia ya mtandao.

“Tuliwasilisha hati ya dharura Mahakama Kuu kulitaka Jeshi la Polisi limpe dhamana Magoti,” alisema Ole Ngurumwa katika mkutano na waandishi wa habari.

“Tunatoa siku moja ya leo (jana) kama watashindwa kufanya hivyo tutaendelea na kesi.”

Alisema Jeshi la Polisi ni chombo kilichowekwa kwa ajili ya ulinzi wa raia na mali zao, hivyo halipaswi kutumika kuwakandamiza.

“Kufuatia kukithiri kwa masuala kama haya, Tanzania tuhuishe mchakato wa Katiba ili kuweka chombo huru kitakachosimamia utendaji na uwajibikaji wa Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama kwa lengo la kulinda haki za wananchi wakiwa mikononi mwa polisi,” alisema.

Naye Henga alisema taasisi hizo zimeamua kufungua kesi kwa kuwa zinamsaka mwenzao.

“Wamechukua uamuzi huu baada ya Jeshi la Polisi kutoweka wazi kituo gani cha polisi alipo mfanyakazi mwenzao,” alisema Henga.

Alisema utaratibu uliotumika kumkamata Magoti si wa kawaida na mwendelezo baada ya kukamatwa si hatua za kiweledi katika utendaji.

Alisema kitendo cha polisi kushikilia watu na kutoa taarifa baada ya kelele za wananchi, si sahihi na kwamba mazingira ya kukamatwa kwa Magoti yanaonekana ya kuvizia, kutumia nguvu kupita kiasi, na bila kupewa haki za msingi kama kuwaarifu watu wake wa karibu.

“Imekuwa ni tabia inayozidi kukua nchini kwa vyombo vya usalama wa raia kukamata watuhumiwa kisirisiri kisha kubaki nao muda mrefu bila ndugu zao kuwa na taarifa,” alisema.

“Mifano ya hivi karibuni ni pamoja na kukamatwa kwa Erick Kabendera (mwanahabari), Maneno Mbunda (wakili) na wengine,” alisema.

Alisema polisi hawana mamlaka ya kumshikilia mtuhumiwa kwa zaidi ya saa 24 bila kumpa dhamana au kumfikisha mahakamani na kuwa haki ya dhamana ni haki ya kikatiba kwa raia yeyote.

“Mambo haya yote yanazua maswali mengi na sintofahamu kwa wananchi na wadau wapenda haki hasa polisi kutoeleza umma na familia mahali alipo mfanyakazi mwenzetu hadi tunapoandika tamko hili siku ya nne,” alisema.

Tukio la kumakatwa kwa Kabendera lilitokea katika mazingira kama hayo baada ya watu kumfuata nyumbani kwake na kumchukua kwa nguvu, lakini taarifa zikaenea kwa kasi mitandaoni zikihofia kuwa alitekwa hadi Jeshi la Polisi lilipotoa kauli kuthibitisha kuwa linamshikilia.

Katika mkutano huo wa jana uliolenga kuzungumzia usalama wakati wa sikukuu, Kamanda Taibu aliwataka wananchi kuzingatia sheria za nchi na kwamba sheria kali zitachukuliwa kwa watakao kiuka.