VIDEO: IGP Sirro akemea polisi kuwahukumu watuhumiwa hadharani

Muktasari:

Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro jana alitumia takribani dakika 70 kukemea, kuonya na kutoa mwongozo, akitaka maofisa wa chombo hicho wafuate dira yake kwa kuwa anayeweza kushika cheo alichonacho ni “mtu mmoja tu” na muda wake ukifika ataondoka.

Dar es Salaam. Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro jana alitumia takribani dakika 70 kukemea, kuonya na kutoa mwongozo, akitaka maofisa wa chombo hicho wafuate dira yake kwa kuwa anayeweza kushika cheo alichonacho ni “mtu mmoja tu” na muda wake ukifika ataondoka.

Hotuba hiyo ya Kamanda Sirro pia iligusia maofisa ambao wamekuwa wakiwahukumu watuhumiwa katika mikutano na waandishi wa habari.

“Huwa nashangaa. Wakati mwingine hivi unamchukua mtuhumiwa, unamuweka pale unamuonyesha kila wakati. Unatafuta sifa?” alihoji.

“Hivi kwenye upelelezi katika mazingira ya kawaida huyo si mtuhumiwa tu? Leo unamtoa hadharani kaiba, unasahau kesho na keshokutwa. Kwenu huko Musoma anakushtaki kwamba kuna siku ulinidhalilisha mimi kuwa mwizi. Vitu vingine tushauriane, si ndiyo.”

Mmoja wa maofisa ambao wamekuwa wakitangaza hadharani watuhumiwa ni kamanda wa Dodoma, Gilles Muroto ambaye huwaonyesha watuhumiwa mbele ya waandishi, kutaja uhalifu anaodai wamefanya na baadaye kusema walikiri katika mahojiano na polisi.

Alishafanya hivyo kwa watu aliodai kuwa ni matapeli na wengine wezi wa njia ya mtandao.

Kamanda Sirro pia alikemea hilo.

“Off course anataka political mileage (umaarufu wa kisiasa), ambayo haistahili kama jeshi,” alisema IGP.

“Angalieni kwenye nchi nyingine ni mara chache sana kukuta mtuhumiwa anaonyeshwa haradhani. Mpaka imetokea jambo kubwa sana ndipo unaweza kufanya. Wanaojua jeshi wanakushangaa. Itafikia unatoa press zako watu wanaona haina maana.”