VIDEO: Kilichomponza Mbowe jimboni hiki hapa

Mwenyekiti wa Chadema na Mbunge wa Jimbo la Hai, Freeman Mbowe akihutubia wananchi wa Kijiji cha Lemira Kati, Kata ya Masama Kati katika Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro juzi, alipoanza ziara ya siku nne kwenye jimbo lake. Picha na Filbert Rweyemamu

Hai. Ujumbe aliotoa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kwenye mkutano wake wa hadhara uliofanyika juzi katika viwanja vya Nkoromu kata ya Masama Kati wilayani Hai umeelezwa ndio sababu ya kukamatwa kwake na polisi akidaiwa kutoa maneno ya uchochezi.

Juzi Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai alikamatwa na polisi baada ya kumaliza mkutano wake saa 11: 58 jioni na kuhojiwa katika Kituo cha Polisi Hai kuanzia saa 12:30 hadi saa 3 usiku.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Salum Hamdun alilieleza Mwananchi kuwa Mbowe amekamatwa baada ya kutoa maneno ya uchochezi katika mkutano huo.

Alisema maneno aliyoyatoa yanaashiria uchochezi na kuamsha hisia za wananchi, chuki dhidi ya Serikali ya Tanzania na polisi.

“Anahojiwa lakini baada ya mahojiano atapewa haki ya dhamana,” alisema Kamanda Hamdun.

Alivyokamatwa

Polisi walimzingira mara baada ya kuteremka kutoka jukwaani na kulazimisha kuingia katika gari lake kwa ajili ya kuongozana naye kwenda kituoni.

Hali hiyo iliibua sintofahamu lakini baadaye Mbowe aliridhia polisi hao kuongozana naye.

Baada ya msafara huo kufika kituoni, Mbowe na msaidizi wake walishuka na kuingia ndani kwa ajili ya mahojiano.

Mbowe ambaye aliingia kwa mahojiano saa 12:35, alitoka saa 3:20 na hakuwa tayari kuzungumza na vyombo vya habari na badala yake aliingia kwenye gari na kuondoka kituoni hapo.

Alichokisema Mbowe

Akizungumza katika mkutano huo, Mbowe aliwaeleza polisi waliokuwepo eneo hilo na silaha za moto kutambua kuwa wana haki ya kuwa katika mkutano wa chama chochote cha siasa, na wana wajibu wa kuwalinda wananchi wa vyama vyote vya siasa, dini zote, kabila zote bila ubaguzi.

“Ndugu zangu Watanzania wa Masama, mna haki ya kuwa chama chochote cha siasa, mtu unaweza kuwa Chadema, ni haki yako kisiasa, unaweza kuwa CCM, ni haki yako kisiasa, au chama chochote cha siasa na polisi wana wajibu wa kuwalinda Watanzania wote bila ubaguzi wa aina yoyote kwa sababu uhuru na umoja wetu unatolewa kama misingi ya katiba ya nchi yetu.”

Alisema hakuna wakati ambapo taifa limepitia kipindi kigumu kama kipindi cha miaka minne na nusu ya utawala wa Rais John Magufuli, ambapo mikutano ya siasa ilizuiwa na wananchi kukosa haki ya msingi ya kuwasikiliza viongozi wao wa kitaifa akiwemo yeye ambaye anaruhusiwa kuongea Hai pekee ilhali yeye ni kiongozi wa kitaifa.

“Mimi ni Mbowe, mwenyekiti wa Chadema wa Taifa, kiongozi wa upinzani bungeni na mbunge wa Hai, ninamuogopa Mungu, simuogopi Magufuli, ninamuheshimu, siogopi polisi ninawaheshimu na ninawapenda, simuogopi mtu yeyote zaidi ya Mungu, lakini namheshimu kila mtu na sipendi kumvunjia mtu yeyote heshima,” alisema Mbowe.

Aliongeza kuwa “Nategemea wenzetu ambao wapo kwenye vyombo vya ulinzi na usalama, ambao wamepewa mamlaka ya kuongoza maisha ya Watanzania, wataliheshimu hilo, watatuona wote kama Watanzania ambao tupo sawa mbele za Mungu na wananchi ambao tuko sawa mbele ya katiba ya nchi, waache taifa letu liishi kwa haki, upendo na lisiwe taifa lililojaa hofu.”

Alisema “Watanzania leo kama vile tuna msiba, kila mahali wamekuwa na woga, tunawaogopa viongozi wetu badala ya kuwaheshimu, tumejenga woga hata kuongea haki zetu za msingi tunaogopa.”

Alisema wakati mfumo wa vyama vingi unaanza, Chadema kilionekana kama chama kidogo cha siasa, lakini wamekijenga kwa wivu na mapenzi makubwa, na kuwaunganisha Watanzania wa makabila yote tofauti na mwanzo walipokiita cha Wachaga kutokana na waanzilishi wake.

“Chama hiki kilivyoendelea kukua walikipa majina mengi ikiwemo chama cha kaskazini, na sasa chama walichokiona mchicha, kimekuwa kama mbuyu, kimekuwa nguvu ya Watanzania wote na kuwa chama kikuu cha upinzani nchini, chenye wabunge mikoa yote ya Tanzania, madiwani na wanachama zaidi ya milioni saba nchini.

“Hiki ni chama ambacho, vigogo wakilala wanaota Chadema, wakiamka wanaota Chadema, wakilala wanamuota Mbowe, kwa wivu mkubwa tumejenga chama ambacho ni tumaini la Watanzania na mwiba kwa CCM,” aliongeza.

Mbowe alisema hawakujenga chama kwa ajili ya kusababisha vurugu, bali wamejenga chama cha kisiasa, chenye sera safi ambacho kinaweza kuwapa Watanzania chaguo mbadala wa CCM.

Hivyo, alisema Chadema inavyozidi kukua ndivyo CCM inavyozidi kusinyaa na Watanzania kuisahau kwa kuwa CCM ya Mwalimu Nyerere siyo ya CCM Magufuli”

“Naomba niwaambie vyombo vya usalama, polisi na wananchi ambao bado ni wanachama wa CCM, Chama chenu kiko Hoi. Bila polisi CCM ni maiti, haipo, CCM ilikuwa wakati wa Mwalimu, kila siku zinavyozidi kwenda chama hiki kinazidi kuzorota na sasa hawawezi kushinda uchaguzi wowote nchini bila kutumia nguvu ya polisi.”

“Tunapenda nchi ya kidemokrasia wananchi wanaopendana wanaheshimiana kila mmoja kwenye nchi hii ajione ana haki na uhuru wa kuwa katika Taifa hili,” alisema.

“Tunataka nchi yenye furaha na amani hapa si Kosovo na Afganistani, askari wanapita wakiwa wamebeba mabomu mnampiga nani mabomu, tunataka askari wetu wachanganyikane na raia, raia waone raha kuja kwenye mkutano na wakiona askari wawakimbilie”