Lissu ashtaki Umoja wa Mabunge Duniani

Makamu mwenyekiti wa Chadema- Bara, Tundu Lissu

Dar es Salaam. Tundu Lissu alifika mbele ya Kamati ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) jijini Geneva, Uswisi ili kuhojiwa juu ya kushambuliwa kwake kwa risasi na kupoteza kiti chake cha ubinge.

Lissu, ambaye ni Makamu mwenyekiti wa Chadema Bara alihojiwa na kamati hiyo jana alasiri baada ya kuwasilisha malalamiko kupitia kwa mwanasheria wake kwenye taasisi hiyo juu ya madhila yaliyomkuta.

Mbunge huyo wa zamani wa Singida Mashariki, amekuwa nje ya nchi tangu Septemba 7, 2017 aliposhambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana akiwa katika makazi yake Area D jijini Dodoma baada ya kutoka kuhudhuria mkutano wa Bunge.

Baada ya kushambuliwa, alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na baadae alihamishiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya alikopata matibabu hadi Januari 6 mwaka juzi alipokwenda nchini Ubelgiji kwa matibabu zaidi na hadi sasa yuko huko.

Licha ya Lissu kudai amepona lakini amekwisha kunukuliwa akisema hatorejea nchini hadi pale atakapohakikishiwa usalama wa maisha yake akijenga hoja kwamba kilichomtokea Septemba 7 mwaka 2017 kililenga kumuua hivyo anahitaji kuwa makini.

Jana, akizungumza na Mwananchi muda mfupi kabla ya kwenda katika kamati hiyo alisema, “Leo (jana) saa 9.00 alasiri kwa saa za Uswisi (saa 7.00 mchana kwa saa za Tanzania), nitakuwa mbele ya kamati ya haki za binadamu ya Umoja wa Mabunge duniani kuzungumzia kushambuliwa kwangu, kuondolewa ubunge na jinsi wabunge wa upinzani wanavyopata wakati mgumu Tanzania.”

“Ninakwenda kwenye hiyo kamati baada ya kuitwa kutokana na kuwaandikia malalamiko kupitia kwa mwanasheria wangu wa Uingereza ambapo sasa wameniita,” alisema.

Rais huyo wa zamani wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) alisema, “licha ya ukweli kamati haiwezi kunirudisha bungeni lakini ni sehemu ya kuionyesha dunia uonevu unaofanywa dhidi ya wabunge wa upinzani wa Tanzania.

Lissu aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki tangu mwaka 2010 alipochaguliwa kwa mara ya kwanza hadi Juni 28 mwaka jana baada ya Spika Job Ndugai kutangaza bungeni kuwa Lissu alikuwa amepoteza sifa za mbunge.

Spika Ndugai alitoa sababu mbili zilizomfanya Lissu kupoteza ubunge ni pamoja na kutotoa taarifa ya wapi alipo na kutokujaza fomu za mali na madeni za sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma.

Uamuzi wa Spika Ndugai ulikwenda sambamba na kumwandikia barua Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kuhusu nafasi hiyo kuwa wazi.

Nec iliitisha uchaguzi mdogo ambapo Miraji Mtaturu alipita bila kupingwa kuongoza jimbo hilo.

Hata hivyo, Lissu alifungua kesi Mahakama Kuu kupinga hatua hiyo ya Spika Ndugai lakini mahakama iliyatupilia mbali maombi yake kwa kile kilichoelezwa na Jaji Sirillius Matupa kuwa mwanasiasa huyo alipaswa kufungua kesi ya kupinga uchaguzi wa jimbo hilo na si uamuzi wa Spika.

Jaji Matupa alisema kama maombi ya Lissu yakikubaliwa yatasababisha uvunjaji wa katiba kwa kuwa italazimika kuwa na wabunge wawili kwenye jimbo moja la Singida Mashariki.