VIDEO: Mashinji aonja shubiri korti ya Kisutu

Tuesday February 25 2020

Wakili Peter Kibatala (Kulia) akiwaeleza jambo

Wakili Peter Kibatala (Kulia) akiwaeleza jambo viongozi wa Chadema wanaokabiliwa na kesi ya uchochezi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam akiwemo aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho ambaye kwa sasa amejiunga CCM, Dk Vicent Mashinji (wa tatu kushoto), baada ya kesi hiyo kupangiwa tarehe nyingine, jijini jana. Picha na Omar Fungo 

By Fortune Francis,Mwananchi [email protected]

Dar es salaam. Aliyekuwa katibu mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji jana alikutana na shubiri mahakamani baada ya kutosalimiana na baadhi ya washtakiwa wenzake, huku wakili anayemtetea akijitoa.

Kwanza alipoingia katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu kusikiliza kesi inayomkabili pamoja na viongozi nane wa Chadema alisalimiana na baadhi ya washtakiwa wenzake, lakini alipofika kwa mbunge wa Kawe, Halima Mdee na kumpa mkono kumsalimia, mbunge huyo hakunyanyua mkono wala kumtazama, bali aliendelea kuchezea simu yake ya mkononi.

Pili alipoingia mahakamani alipishana na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, jambo lililosababisha ashindwe kusalimiana naye.

Tatu, John Mallya ambaye ni wakili aliyekuwa akimtetea alijitoa kumtetea katibu mkuu huyo wa zamani wa Chadema ambaye Februari 18 alihamia CCM ikiwa ni miezi miwili tangu Mbowe alipomteua mbunge wa Kibamba, John Mnyika kuwa katibu mkuu wa Chadema.

Dk Mashinji alikuwa katibu mkuu wa Chadema kuanzia Februari 2016 hadi Desemba 18, mwaka jana.

Mashinji alifika mahakamani hapo akiwa kwenye gari ndogo aina ya Toyota Premio kisha kuingia mahakamani walipokuwa wamekaa washtakiwa wenzake na kuanza kuwasalimia akiwemo mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, lakini hali ilikuwa tofauti alipofika kwa Mdee ambaye hakumpa mkono wa kumsalimia.

Advertisement

Baadaye Mdee alipoulizwa na Mwananchi sababu za kutomsalimu Dk Mashinji alisema kwa kifupi, “...,achana naye huyo ni mnafiki.”

Dk Mashinji pia alikwama kusalimiana na Mbowe baada ya kupishana katika chumba cha mahakama.

Mbowe alikuwa mshtakiwa wa mwisho kuingia katika chumba cha mahakama na kukuta washtakiwa wengine wakiwa wamekaa na kupita moja kwa moja kwenda kukaa.

Baada ya kesi kuanza washtakiwa walipanda kizimbani, huku Mbowe akikaa kiti cha mbele na Mashinji nyuma na baada ya kesi kuahirishwa alianza kutoka na Dk Mashinji akifuata nyuma.

Awali akitambulisha jopo la mawakili, Wakili wa utetezi Peter Kibatala alisema yeye na Wakili Fredy Khiwelo wanatetea watuhumiwa wote isipokuwa wakili John Mallya ambaye hamtetei mshtakiwa wa sita (Dk Mashinji).

“Mimi na Wakili Fredy Khiwelo tunawatetea washtakiwa wote, Wakili John Mallya anawatetea washtakiwa wote isipokuwa mshtakiwa wa sita,”alidai Kibatala.

Hata hivyo, mahakama imepanga Machi 10 kutoa hukukumu katika kesi hiyo namba 112 ya mwaka 2018 inayowakabili viongozi hao.

Uamuzi huo ulitolewa na hakimu mkazi mkuu, Thomas Simba wakati kesi hiyo ilipofika kwa ajili ya kufanya majumuisho.

“Kesi itakuja Machi 10 kwa ajili ya hukumu majumuisho yanatakiwa kuwasilishwa mahakamani kwa njia ya maandishi katika siku tano za kazi kuanzia leo,” alisema hakimu Simba.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine ni Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu, Salum Mwalimu, Mwenyekiti wa Bawacha, Halima Mdee.

Wengine ni Mnadhimu wa kambi ya upinzani bungeni, Ester Bulaya, Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa, Peter Msigwa, Mbunge wa Tarime vijijini, John Heche na Mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti, Ester Matiko.

Advertisement