Walichokisema wananchi kuhusu Makamba, Kinana

Tuesday July 16 2019

 

By Exaud Mtei, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Wananchi wametoa  maoni tofauti kuhusu malalamiko yaliyowasilishwa na makatibu wakuu wawili wa zamani wa CCM, Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana wanaodai kudhalilishwa kwa mambo ya uzushi, uongo na mtu aliyejitambulisha kuwa mwanaharakati na mtetezi wa Serikali.

Wananchi hao wametoa maoni hayo kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii ya Mwananchi kupitia swali lililosema; Nini maoni yako kuhusu barua ya waliokuwa makatibu wakuu wa CCM kwenda kwa katibu wa baraza la ushauri la viongozi wastaafu wa chama hicho wakilalamikia tuhuma wanazopewa, mhusika kutochukuliwa hatua.

Wawili hao walituma malalamiko hayo kwa kuzingatia katiba ya CCM, toleo ya 2017 ibara ya 122, wakisema madai ya mwanaharakati huyo yanahatarisha umoja, mshikamano na utulivu ndani ya chama hicho tawala nchini Tanzania.

Katika mtandao wa kijamii wa facebook, Anna Mwasubila  amesema japokuwa viongozi hao wamechelewa kuandika barua hiyo, wamefanya vyema kuchukua uamuzi huo.

“Wamefanya vyema li tuone matokeo ya hiyo barua, maana isije ikawa wameandika halafu wamalizane kimyakimya,  mrejesho ni muhimu,” amesema Mwasubila.

Kwa upande wake, Alex Paul kupitia mtandao huo wa kijamii amesema, “Huko walikokwenda wanatafuta huruma tu na kujaribu katisha mamlaka. Kama wanaona wamekosewa haki, wana machaguo mawili tu, wapotezee na kukaa kimya au waende mahakamani kama mwenzao alivyofanya.”

Advertisement

John Swedi amesema wastaafu hao walitumika wakati wa Julius Nyerere na kutaka waheshimiwe.

Steven Mdoe amesema ubatizo wa moto umefikia zamu yao, “Mimi nawashauri watulie kimya waendelee kupata haki yao maana hawa ndio waasisi wa ubatizo wa moto.”

Kwa upande wake, Batchi Vitalis amesema wakati mwanaharakati huyo alipokuwa akisoma majina ya wapinzani  wanatumika na mabeberu, makatibu hao hakuwasikia kuandika barua kwa chama chao kuomba mwongozo.

“Sasa imefika zamu yao wanaandika barua na malalamiko kibao, hii ni zamu yao walidhani wako salama zaidi ya wapinzani. Huu ni ubatizo wa moto, tulieni mbatizwe,” amesema Vitalis.

Prosper Kamuzora Vedasto amesema, “Ni wakati wa kujitafakari kama hatuna wazee wa kukemea uovu nchini basi tunajenga Taifa lisilo na maadili. Huwezi kuletewa mashtaka na kumwambia anayelalamika aende kujibu mapigo, huo ni upungufu mkubwa wa nidhamu katika jamii kuruhusu watu kujichukulia sheria mikononi.”

Edward Chilangwa amesema, “Wapumzike. Wasihangaike italipa. Kama hawako kwenye uovu basi ukweli utawaacha huru. Wakihangaika vijana wa leo hawana simile watachimba uovu, makosa na kuanika.

Wanyamaze lakini wasiingilie nguvu mpya. Waige Wakuu wengine. Angalia mtazamo wa 2015 tuu umeshakuwa zama za kale.”

Remmy Akarro amesema, “Kuchafuana si ustaarabu kwa pande zote zenye maslahi na chama na Serikali, watulie, kubatizana huko sio heshima na wala sio vizuri.”

“Wakae kimya kama ambavyo walinyamaza pale Lissu (Tundu) alipopigwa risasi, Saanane (Ben-msaidizi wa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe), Azory (Gwanda-mwandishi wa kujitegemea wa gazeti la Mwananchi) walipopotea na Mo (mfanyabiashara Mohammed Dewji) alipotekwa na Membe (Bernard- Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje) alipochafuliwa, kipi kinawafanya wapige kelele,” amesema Embeghwa Mnyanyuda akiwataka waendelee kukaa kimya kwa kuwa matukio hayo yalipotokea hawakusema chochote.

Katika mtandao wa kijamii wa Twitter

Emmanuel Mturo ameandika, “Kulikuwa hakuna ulazima wa kuandika barua ya wazi kabla hawajalipeleka (suala hilo) mbele ya baraza la wazee lipatiwe ufumbuzi huko kama kuna ugumu wowote basi barua hiyo ingekua na muda muafaka wa kuitoa wazi.”

Advertisement