Vigogo wazungumzia kitabu cha Mkapa

Moshi/Dar es Salaam. Vigogo wa siasa nchini wamemsifu Rais Benjamin Mkapa wa Serikali ya Awamu ya Tatu kwa kuandikia kitabu kuelezea matukio ya enzi za utawala wake, huku baadhi wakiitaka CCM itafakari aliyoyasema.

Katika kitabu chake cha “My Life, My Purpose (Maisha Yangu, Kusudi Langu)” alichozindua Jumanne, Mkapa ameongelea masuala mbalimbali ya siasa, kiuchumi na kijamii, akijutia baadhi ya mambo yaliyotia dosarti utawala wake, huku akisifu misimamo iliyomsaidia kunyoosha njia.

Kisiasa amezungumzia utawala bora, demokrasia na jinsi ya kushirikiana na wapinzani katika mustakabali wa Taifa.

Pamoja na kuzungumzia historia yake na miaka 10 ya uongozi wake kama Rais, Mkapa ameshauri kwa kirefu jinsi ambavyo CCM inatakiwa kubadilika na namna inavyoongoza nchi akihimiza haja ya vyama vya siasa kufanya kazi kwa uhuru na pia kujengwa kwa uchumi wa kunufaisha wananchi walio wengi.

Ujumbe wake katika kitabu hicho umepokewa kwa mtazamo chanya na viongozi tofauti waliohojiwa na Mwananchi, wengi wakimsifu kwa kuchambua na kukiri makosa ya uongozi wake na pia kitendo cha kukosoa baadhi ya mambo ambayo hayaendi sawa.

“Mkapa ameonyesha ujasiri na uwezo mkubwa katika dhamana ya uongozi na kuna umuhimu mkubwa wa kujifunza kutoka kwake,” alisema Kanali Ngemela Lubinga, katibu wa Halmshauri Kuu ya CCM (siasa na uhusiano wa kimataifa).

“Ametufundisha na amefungua ukurasa mpya wa mtu kuandika historia, kuzungumzia majukumu yake na pia kukiri kuwa kuna mahali aliyoyataka hayakutekelezwa.

“Kukiri kuwa kuna mambo hakuyafanya vizuri ndio uongozi. Anawakomaza vijana waelewe namna ya kufanya yanayostahili. Ameweka historia kuwa kulikuwa na viongozi wenye uwezo na walioweka miongozo ya kuongoza Tanzania.”

Hata hivyo, kuhusu kuwepo kwa tume huru ya uchaguzi, Kanali Lubinga alisema baadaye jana jioni kuwa Mkapa hakuweka bayana suala hilo.

“Tume huru ya uchaguzi ipo kwa kuwa imewekwa kisheria,” alisema.

“Labda angetushauri tume huru iweje kwa kuwa vyama vinashiriki kuhesabu kjura kama alivyosema.”

Hata hivyo, Mkapa, ambaye amezungumzia uongozi wa Afrika kwa ujumla, alisema tume huru ni ile inayoshirikisha vyama vyote na inayofanya kazi kwa uwazi na kwamba enzi zake tume iliaminika kwa kuwa aliteua jaji aliyekuwa anaaminika, lakini matatizo yalikuwa katika kuhesabu kura na kutangaza washindi.

Mwingine aliyezungumzia kitabu hicho ni mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Vyama vya Siasa, John Shibuda aliyeunga mkono ushauri wa Mkapa kwa CCM kujiondoa katika kasumba ya kujiona ipo kwenye mfumo wa chama kimoja.

Shibuda alisema kitabu hicho kinapaswa kuwa ni sabuni ya kusafisha dosari kwa viongozi wa kizazi cha sasa wanaotafuta elimu kutokana na ujuzi wa wazee.

“Kwa kuwa wanasema uzee ni dawa au kuishi kwingi kuona mengi, mheshimiwa Mkapa kitabu chake ni shamba darasa kwa viongozi kutambua sababu zilizosababisha dosari katika uongozi wake.

“Watanzania tufurahi kwamba tumepata kitabu ambacho kina sifa ya kuwa darubini ya kupambanua desturi za utumishi bora. Kinatukumbusha uwajibikaji wa maadili sahihi,” alisema Shibuda.

Shibuda ameitaka Serikali ya CCM ijitathmini na ichukizwe na desturi za tabia za kujihisi ina thamani ya kuitwa ina hati miliki ya nchi.

“(CCM) Wana kasoro ya kuhisi bado tuko katika mfumo wa chama kimoja cha siasa. Mkapa ametoa wito kwa uongozi mkuu wa CCM uondokane na dhambi ya ubaguzi ambayo Baba wa Taifa aliikemea,” alisema Shibuda, ambaye ni kada wa zamani wa CCM.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alitaja jambo lililomvutia katika kitabu hicho kuwa ni pale Mkapa alipozungumzia maridhiano.

“Kitu kilichonipendeza zaidi ni kitendo cha Mkapa kuzungumzia suala la watu kukaa pamoja kwa maridhiano. Kujitambua kuwa na mawazo tofauti ni jambo linafaa zaidi na kuvumiliana pia,” alisema Mbatia.

Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alisema amefurahishwa na namna Mkapa alivyofunguka na kuonyesha kutoridhishwa na hali ya demokrasia ilivyo nchini.

Zitto alisema kitabu cha Mkapa kimempa majawabu ya mambo yaliyokuwa yakimsumbua alipochaguliwa kuwa mbunge, alipodhani utawala wake ulikithiri kwa rushwa.

“Nilikuwa naumizwa sana na hali ya umasikini na namna rasilimali madini zilivyokuwa zinaporwa. Nilikuwa nikimtazama Mkapa kama kiongozi asiyejali watu maskini aliyeuza nchi kwa wageni,” alisema Zitto.

“Kitabu chake kimeweza kunipa majawabu ya baadhi ya mambo niliyokuwa najiuliza wakati ule. Kwa mfano suala la ubinafsishaji wa mashirika ya umma na namna lilivyotekelezwa.”

Zitto alisema ameridhika na maelezo ya Mkapa yaliyomo katika kitabu hicho kuhusu mageuzi makubwa aliyoyafanya kwenye uchumi, lakini hakubaliani na ulazima wa ubinafsishaji.

“Rais Mkapa alipaswa kuachia sekta binafsi kushindana na mashirika ya umma badala ya kuwauzia watu kwa bei ya kutupwa na mashirika kutoendelezwa,” alisema Zitto.

Zitto alitoa mfano wa China kuwa hawakuuza mashirika, bali waliruhusu sekta binafsi kushindana na mashirika na matokeo yake yakawa chanya.

Pia Zitto alizungumzia suala la wizi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (Epa) ya Benki Kuu (BoT), akisema Mkapa amekiri wazi juu ya wizi huo.

“Hili Mkapa ametendea haki nchi, lakini alipaswa kwenda hatua ya pili na kuomba radhi kwa kuruhusu wizi wa namna ile ambao ulikuwa na madhara makubwa kwa nchi yetu,” alisema.

Katika sakata hilo, Mkapa ameeleza jinsi ambavyo alishauriwa vibaya kuhusu fedha zilizokuwa katika akaunti hiyo ambazo zilichukuliwa na wafanyabiashara walioghushi barua kuonyesha kuwa wamemilikishwa madeni na kampuni za nje na hivyo kuomba walipwe.

Sakata hilo lililipuka wakati wa utawala wa kiongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, ambaye aliwataka waliochota fedha hizo kuzirejesha ndani ya muda maalum na wale ambao wangeshindwa wafikishwe mahakamani.

Zitto pia alizungumzia mauaji ya wafuasi 22 wa CUF kisiwani Pemba Januari 2001, akisema pamoja na Mkapa kukiri dosari hizo, alipaswa kwenda mbali na kuomba radhi wananchi kwa tukio lile.

“Tume ya uchunguzi ya mauaji yale chini ya Brigedia Jenerali Mstaafu Hashim Mbita ilithibitisha vifo vya watu 35. Taarifa ya chama cha wananchi CUF ilikuwa na watu zaidi ya 60 waliouwawa.

“Serikali ya Mkapa ililipa fidia kwa familia za wafiwa. Hata hivyo nilitarajia kuwa Mkapa angeomba radhi kwa wananchi na pia sikuona habari ya mauaji ya Mwembechai,” alisema Zitto.

Zitto alisema Mkapa sasa anapaswa kukemea yanayoendelea nchini, hasa ukandamizaji wa demokrasia na kuwatenga wapinzani.

“Ameonyesha kuumizwa na mambo hayo kwenye kitabu, lakini hakemei katika sura ya mwisho ya kitabu chake. Kama Rais mstaafu anapaswa kusema na kuonya,” alisema Zitto.

Mfanyabiashara maarufu nchini, Ali Mufuruki amesema amefurahishwa na kitabu hicho kwa kuwa Mkapa amekuwa muwazi kuzungumzia mambo anayoyakumbuka kwenye siasa na hata mambo yake binafsi ya dini na familia.

“Kama mtu ambaye nina struggle (ninapambana) kuandika kitabu, nimekuwa encouraged (nimehamasika) na nimepata funzo kuhusu mambo muhimu wakati wa kuandika autobiography (kitabu cha wasifu wa mtu),” alisema mfanyabiashara huyo maarufu na ambaye ni mwenyekiti mtendaji wa kampuni ya Infotech.

“Mkapa amekuwa muwazi sana kwa kuandika mambo yake mazuri, mabaya, mafanikio na hata yale yaliyomshinda.

“Na hajaandika mambo yote, ameandika yale anayoyakumbuka tu. Kwa kweli kimenifurahisha sana maana ameandika kama mtu mzima, yaani baba na pia kiongozi wa kisiasa.”