Viongozi CUF wamlalamikia Lipumba uchaguzi uliopita Ukawa iliwavuruga

Profesa Lipumba akikagua ujenzi wa ofisi ya chama hicho kata ya Usule Jimbo la Swola wilaya ya Shinyanga vijijini.

Muktasari:

Viongozi wa Chama cha Wananchi CUF Wilaya ya Shinyanga wamemlalamikia mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba kuwa uchaguzi uliopita Umoja wa Katiba ya Wananchi(Ukawa) ndio waliowavuruga.


Shinyanga.Viongozi wa Chama cha Wananchi CUF Wilaya ya Shinyanga wamemlalamikia mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba kuwa uchaguzi uliopita Umoja wa Katiba ya Wananchi(Ukawa) ndio waliowavuruga.

Akiongea leo Oktoba 3, 2019 wakati wa ziara ya Mwenyekiti huyo Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CUF jimbo la Swolwa, Maige Luhaga amesema viongozi wengi walikimbilia Chadema wakiamini Ukawa ni chama kimoja.

"Mwaka 2005 viongozi wetu waliokuwa waanzilishi walikimbilia Chadema wakagombea na kushinda wakiamini ni chama kimoja,"alisema Luhaga

Alisema mwanzo walikuwa na wenyeviti watano lakini baada ya viongozi hao kuhamia Chadema walishinda na CUF kubakiwa na mwenyekiti mmoja.

Luhaga ambaye pia ni mjumbe wa mkutano mkuu amesema kwa sasa wamejipanga kuwa na wenyeviti wa vijiji na vitongoji.

Kwa upande wa Lipumba amesema kwa sasa CUF imejipanga kushiri chaguzi zote kuanzia uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu ujao.

"Tunaenda kuingia kwenye uchaguzi tutashiriki chaguzi zote kuanzia serikali za mitaa hadi uraisi,"ameaema Lipumba.