Vipengele vitatu vyaongezwa tuzo za Ejat

Katibu mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga 

Muktasari:

  • Baraza la Habari Tanzania (MCT) limeongeza vipengele vitatu vya Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (Ejat) mwaka 2019.

Dar es Salaam. Baraza la Habari Tanzania (MCT) limeongeza vipengele vitatu vya Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (Ejat) mwaka 2019.

Vipengele hivyo ni habari  zinazohusu hedhi salama,  ubunifu na maendeleo ya watu na afya ya uzazi.

Hayo yameelezwa leo Ijumaa Oktoba 11, 2019 na katibu mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga  katika uzinduzi wa tuzo hizo.

Mukajanga amesema kundi la tuzo za habari za usalama na ubora wa chakula, kodi na mapato  pamoja na afya yameondolewa baada ya kukosa wadhamini.

Kutokana na kuondolewa kwa vipengele hivyo, vimeongezwa vingine vitatu na kufanya jumla ya vipengele vitakavyoshindaniwa kuendelea kuwa 20.

"Tuzo hizo zimekuwa na mafanikio makubwa ndani ya miaka 10 iliyofanyika. Ejat imeongeza hamasa na ubora wa kazi za waandishi wa kike, Ejat imeibua waandishi wengi wasiojulikana," amesema Kajubi.

"Mafanikio hayo yanaendana na malengo ya Ejat ambayo ni kujenga hamasa ya kuibua waandishi bora na kuhamasisha uandishi wenye maudhui yenye matokeo chanya kwa jamii. "

Kwa mujibu wa MCT, waandishi wanatakiwa kujaza fomu za ushiriki wa tuzo hizo kuanzia leo hadi ukomo wake Januari 31, 2020. Tarehe ya kutolewa kwa tuzo hizo itatangazwa hapo baadaye.