VIDEO: Vyama 11 vya upinzani vyatangaza kushiriki uchaguzi Serikali za mitaa

Mwenyekiti wa DP, Abdul Mluya akizungumza na wanahabari leo.

Muktasari:

Vyama 11 vya upinzani visivyo na uwakilishi katika Bunge la Tanzania vimetangaza kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019 vikieleza kuwa, “anayesusa chakula ameshiba.”

Dar es Salaam. Vyama 11 vya upinzani visivyo na uwakilishi katika Bunge la Tanzania vimetangaza kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019 vikieleza kuwa, “anayesusa chakula ameshiba.”

Vimetangaza uamuzi huo leo Ijumaa Novemba 8, 2019 jijini Dar es Salaam siku moja baada ya Chadema kujitoa kushiriki uchaguzi huo kutokana na figisufigisu zilizofanyika katika uchukuaji, urejeshaji wa fomu za kugombea na uteuzi wa wagombea.

Vyama hivyo ni DP, NRA, AFP, Demokrasia Makini, UDP, ADC, Ada- Tadea, Sauti ya Umma (Sau), TLP, CCK na UMB

Vimesema vitashiriki vikiamini Wizara ya Tamisemi inayosimamia uchaguzi huo itatenda haki kwa kuwarejesha wagombea wake walioenguliwa kushiriki uchaguzi huo.

“Tunaamini watarudishwa kwa sababu wamekidhi matakwa. Tunataka tushindane kwa hoja na sera kwenye mikutano ya hadhara,” amesema katibu  mkuu wa DP,  Abdul Mluya kwa niaba ya viongozi wa vyama hivyo.

Amesema, “tutaendelea na uchaguzi kwa sababu siku zote anayesusa chakula ameshiba. Hatuwezi kususia uchaguzi kwa sababu ni mtaji  wa kujiimarisha hasa kwa vyama hivi ambavyo havina diwani wala wabunge tofauti na Chadema.”

“Ili tuondokane na vyama vya mfukoni visivyo na nguvu njia sahihi ya kufanya ni kushiriki uchaguzi. Tushiriki uchaguzi ili kujenga mizizi kwenye Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji ndio mtaji wa kupata wabunge,” amesema Mluya.