Wabunge wahoji mambo nane Bunge likiridhia azimio kulinda haki miliki

Muktasari:

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya  Kilimo, Mifugo na Maji imehoji mambo nane  kabla ya kuridhia Azimio la Bunge la Itifaki ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) kuhusu kulinda haki miliki za wagunduzi wa aina mpya za mbegu za mimea.


Dodoma. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya  Kilimo, Mifugo na Maji imehoji mambo nane  kabla ya kuridhia Azimio la Bunge la Itifaki ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) kuhusu kulinda haki miliki za wagunduzi wa aina mpya za mbegu za mimea.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Suleiman Ahmed Sadiq amesema bungeni jana Jumatano Septemba 11, 2019 kuwa kamati ilihitaji ufafanuzi wa mambo hayo kabla ya kufikia muafaka.

Kati ya mambo hayo ni nchi zenye uchumi mkubwa katika kilimo zikiwemo Afrika Kusini, Mauritius na Shelisheli kutosaini azimio hilo, kuhoji sababu za Tanzania kuwa na haraka kusaini.

"Tulihoji kuna haraka gani kuridhia wakati ni nchi saba tu kati ya 15 wanachama wa Sadc ndio zimesaini na je haiwezi kusababisha ukiritimba kutoka katika kampuni kubwa za mbegu," amehoji Sadiq.

Amesema nyingine ni vituo vya haki bunifu vya Aripo (Zimbabwe),Oapi cha Afrika Magharibi na Paipo kilichopo chini ya Umoja wa Afrika kama havitaweza kusigana na Itifaki hiyo na kuhoji ni kwa kiasi gani uhuru wa mkulima mdogo katika uzalishaji mbegu umezingatiwa.

Kamati hiyo pia imehoji kwa kiasi gani nchi imewekeza katika tafiti za mbegu ili kumudu ushindani wa nchi wanachama wa Sadc katika ugunduzi, uzalishaji na biashara ya mbegu.

 

Amesema kamati ilihofu kiasi gani itifaki itazingatia tofauti wa maendeleo ya kiuchumi kwa nchi wanachama wa jumuiya hiyo na sababu zipi za kuridhia wakati Tanzania ambayo ni Jumuiya ya Afrika Mashariki inaridhia kitu ambacho hakipo katika jumuiya hiyo.

 

Amebainisha kuwa maswali hayo kwa ujumla wake yalitolewa majibu na Serikali  hivyo wakakubaliana na azimio hilo akisema ni kwa faida ya Taifa, wagunduzi na wakulima.

 

"Pamoja na kukubaliana na azimio, kamati inaomba Serikali itenge fedha za kutosha kwa ajili ya vituo vya utafiti ili kuwezesha watafiti kufanya kazi kwa kutumia fedha za ndani badala ya kutegemea wafadhili kutoka nje," amesema.

 

Ushauri mwingine walitaka Serikali ifanye mapitio na maboresho ya sheria kulinda haki miliki za wagunduzi wa aina mpya za mbegu za mimea ya mwaka 2012 ili waweze kujumuisha maudhui ya itifaki ya maendeleo.

 

Akiwasilisha Azimio hilo Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga amesema mgunduzi atakuwa na haki ya kuidhinisha uzalishaji wa mbegu husika, kuuzwa, kusafirishwa na kuhifadhiwa.

 

Amesema sehemu ya tano ya azimio hilo limetaja muda wa haki miliki utakaotumika  chini ya itifaki hiyo itadumu kwa miaka 25 huku ikiweka zuio kuwa ni kinyume cha sheria kwa mtu mwingine kutumia mbegu yenye haki miliki kibiashara bila idhini ya mgunduzi.

 

Kwa mujibu wa Hasunga, itifaki hiyo itawezesha kuwa na mfumo thabiti wa kulinda haki miliki za wagunduzi wa aina mpya za mbegu za mimea, kuhamasisha ugunduzi wa aina mpya za mbegu za mazao ya kilimo na kutoa haki miliki kwa wagunduzi wa aina mpya za mbegu za mimea.

 

Msemaji wa Kambi ya upinzani,  Pascal Haonga amesema wapinzani hawana shida na azimio hilo, kushauri Serikali kubeba jukumu la kuwaandaa watu wake katika soko la mbegu huku akionyesha mashaka yake kuhusu mbegu za asili kupotea.

 

Haonga amesema bila kuwa makini katika azimio hilo, umilikishaji huo utatoa maana kwamba mnyororo mzima wa mbegu unakuwa ni kwa faida ya wagunduzi waliosajiliwa na kutambuliwa.