Wafanyabiashara 15 kortini kwa kukosa mashine za EFD

Friday August 16 2019

 

By Joseph Lyimo, Mwananchi [email protected]

Babati. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoani Manyara, imewafikisha mahakamani wafanyabiashara 15 wa Mjini Babati nchini Tanzania  wakidaiwa kufanya biashara bila kuwa na mashine za kutoa risiti za kielektroniki (EFD).

Meneja wa TRA mkoani Manyara, John Mwigura akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Agosti 16,2019 amesema wafanyabiashara hao wamefikishwa kwenye mahakama ya hakimu mkazi wa wilaya ya Babati.

Mwigura amesema wafanyabiashara hao ni wale wenye kuuza mauzo ghafi ya Sh14 milioni na zaidi kwa mwaka.

Amesema mashine ya EFD inawahusu wafanyabiashara ghafi wanaouza Sh38,000 kwa siku sawa na Sh14 milioni kwa mwaka.

"Wafanyabiashara hao ni wale wanaouza mauzo ghafi siyo mtaji wa Sh14 milioni lazima waelewe hilo mfano mtu unauza kilo saba kwa siku buchani lazima uwe na EFD," amesema Mwigura.

Hata hivyo, amesema baadhi ya wafanyabiashara hao baada ya kufikishwa mahakamani wameomba wakutane nao faragha nje ya mahakama ili wazungumze juu ya hilo.

Advertisement

 

"Sisi lengo letu ni kutimiza wajibu wetu hatuna ubaya na mtu, baada ya kuwapeleka mahakamani baadhi yao wanataka tukutane tuzungumze ili watekeleze kwa kufunga mashine hizo," amesema Mwigura.

Amesema mfanyabiashara anayepaswa kuwa na mashine ya EFD siyo lazima awe na biashara kubwa ili mradi awe anafanya mauzo ya Sh38,000 kwa siku.

"Elimu tumeitoa kwa muda mrefu na wafanyabiashara wameipata na wengine tuliwaandikia barua kuwa wana sifa za kuwa na EFD lakini hawana mashine hizo," amesema Mwigura.

Amesema waliwapa taarifa wafanyabiashara wenye kuwa na kikwazo cha kutokuwa na mashine hizo wafike ofisini kwao wajadili hilo lakini hawakutekeleza.

Amesema walitoa mwezi mmoja kwa wafanyabiashara hao ambao hawajafunga mashine hizo na wakawaeleza kuwa watawafikisha mahakamani wasipotimiza hilo.

Mmoja kati ya wafanyabiashara hao wa mjini Babati, John Tluway amesema wengine walidhani jambo hilo halitafika mahakamani ndiyo sababu hawakutimiza hilo.

"Tulipewa elimu kupitia vikao mbalimbali juu ya mashine ya EFD na pia magari ya matangazo yalikuwa yanasisitiza juu ya kununua mashine hizo ila utekelezaji wake kwa baadhi kudharau hilo," amesema Tluway.

Advertisement