Wagombea urais wajinadi kwa mazuri ya Nyerere

Muktasari:

Nyerere aliiongoza Tanzania kuanzia mwaka 1961 hadi 1985 kabla hajafariki dunia Oktoba 14 mwaka 1999 nchini Uingereza alikokuwa anatibiwa hivyo kila mwaka Taifa kuienzi tarehe hiyo.

Dar/mikoani. Wagombea watatu wa urais wametumia sehemu ya kampeni zao kueleza namna vyama vyao vinavyodumisha na kuenzi mazuri yaliyofanywa na Rais wa kwanza, Julius Nyerere ambaye jana ilikuwa kumbukumbu ya miaka 21 ya kifo chake.

Nyerere aliiongoza Tanzania kuanzia mwaka 1961 hadi 1985 kabla hajafariki dunia Oktoba 14 mwaka 1999 nchini Uingereza alikokuwa anatibiwa hivyo kila mwaka Taifa kuienzi tarehe hiyo.

Wagombea walijinasibisha na Nyerere jana ni Dk John Magufuli (CCM), Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) na Tundu Lissu (Chadema) pamoja na mgombea mwenza wake, Salum Mwalimu.

Alichokisema Magufuli

Katika mkutano alioufanya jana kwenye viwanja vya Tanganyika Packers jijini Dar es Salaam, Magufuli aliwataka Watanzania kuendelea kumuenzi Nyerere kwa kudumisha tunu tano alizoziacha.

“Kuna mambo mengi ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, kubwa ni kutujalia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuzaliwa Tanzania. Alikuwa mtu wa pekee sana kwa uongozi bora, sio Tanzania pekee bali Afrika na duniani kote,” alisema Magufuli.

Alisema Nyerere anakumbukwa Tanzania, Afrika na ulimwenguni kote kwa kuamini umoja, usawa, kuheshimiana na kujitegemea.

Akimuhusisha na uchaguzi mkuu, aliwaasa Watanzania kuchagua viongozi watakaoenzi mema aliyosimamia Baba wa Taifa.

Katika tunu tano za Mwalimu, aliitaja ya kwanza kuwa ni uhuru wa Tanzania Bara mwaka 1961.Ingawa Mwalimu aliongoza mapambano ya kuikomboa nchi, Nagufuli alisema alihakikisha uhuru huo unalindwa.

Tunu nyingine Magufuli alisema Nyerere anakumbukwa kwa kuamini katika amani na utulivu, sifa aliyoiachia Tanzania. Alisema Nyerere alijihusisha kimataifa mfano usuluhishi wa mgogoro wa Burundi.

Tunu ya tatu alisema ni umoja na mshikamano. Sifa ya Mwalimu alisema ilikuwa kujenga Taifa lenye umoja na mshikamano inayoruhusu watu kuishi bila kubaguana kwa rangi, dini au kabila. Alifanikiwa nchi na akaiunganisha Afrika pia.

“Mwalimu aliunda Taifa ambalo watu wote wanajitambua kama Watanzania,” alisema Magufuli aliyemaliza mzunguko wa tano.

Jambo la nne Magufuli lililoachwa na Mwalimu alisema ni Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliofanyika Aprili 26 mwaka 1964.

Muungano huo ulifanyika baada ya maridhiano kati ya Mwalimu Nyerere aliyekuwa Rais wa Tanganyika na mwenzake wa Zanzibar, Hayati Abeid Karume.

Magufuli aliitaja tunu ya tano kuwa ni misingi ya Tanzania kuwa Taifa linalojitegemea. Alisema Mwalimu aliamini Tanzania ni tajiri wa rasilimali hivyo akahimiza watu kufanya kazi ili kupiga hatua za kimaendeleo.

Ili kutimiza ndoto ya Tanzania kujitegemea, alisema Mwalimu alianzisha mashirika kama vile ya simu, ndege, madini ranchi za Taifa na kujenga viwanda.

Katika mkutano huo, Magufuli aliwaombea kura wagombea ubunge wa CCM akiwamo Askofu Josephat Gwajima (Kawe) na Abbas Tarimba (Kinondoni).

Lissu amkumbuka Nyerere

Akiwa wilayani Ukerewe, Lissu alisema Chadema wanamuenzi Nyerere kwa vitendo katika kulinda uhuru, haki na maendeleo.

Lissu ambaye alikwenda visiwani humo licha ya changamoto ya usafiri baada ya kupanda mtumbwi kutokana na kivuko kutofika, alisema mwaka 1968, Mwalimu Nyerere aliandika kitabu cha “uhuru na maendeleo” alichodai kuwa alifafanua maendeleo ni ya watu si vitu.

“Baba wa Taifa ameeleza katika kitabu chake maana ya maendeleo kuwa ni uhuru wa watu kujiamulia mambo yao hata kama hayawaingizii pesa.”

“Sisi Chadema tunamuenzi Baba wa Taifa ndiyo maana ilani yetu ya uchaguzi inazungumzia uhuru, haki na maendeleo ya watu,” alisema.

Katika kumuenzi Mwalimu Nyerere, Lissu alisema walipanga kwenda Butiama kutoa heshima zao mahali alipolala mwasisi huyo wa Taifa lakini walikataliwa kwa madai kwamba hiki ni kipindi cha uchaguzi.

“Kumuenzi Baba wa Taifa siyo tu kwenda kutoa heshima katika kaburi lake bali kuyaishi maono yake kama ambavyo Chadema tunafanya,” alisema Lissu anayeendelea na kampeni mkoani Mwanza.

Alichokisema Lipumba

Akihutubia wananchi katika Viwanja vya Mwembetogwa mkoani Iringa, Lipumba aliwataka wanasiasa nchini kufuata nyayo za Nyerere kwa kuyaenzi mazuri aliyoyafanya bila upendeleo.

“Tunamkumbuka Mwalimu Nyerere kwa misingi aliyowekeza katika umoja wa kitaifa na kupambana na rushwa.”

“Wakati wa uhai wa mwalimu Nyerere hakuweza kutumia nafasi aliyokuwa nayo kuwapa upendeleo ndugu zake wala familia yake ukilinganisha na viongozi wa siku hizi ambao familia zao wanazipa fursa za uongozi kwenye mamlaka za kisiasa hata wasio na historia ya siasa,” alisema Profesa Lipumba.

Profesa Lipumba alisema Nyerere alikufa kifo cha kawaida hivyo kumbukizi yake ingefanyika siku aliyozaliwa kwa sababu “ndio tulipata mwasisi na baba wa Taifa letu.”

Wakati wote alisema Mwalimu alisisitiza umoja na haki za binadamu, alipambana na rushwa na hakumpa nafasi ya uongozi mke au watoto wake ukilinganisha na viongozi wengine.

Mwalimu amkumbuka Nyerere

Katika mkutano alioufanya Jimbo la Sumbawanga Mjini, Salum Mwalimu aliwataka Watanzania kutafakari maisha ya nyuma na kule wanakotamani kuwa kisha wachukue hatua Oktoba 28.

“Kumbukizi ya Nyerere tuitumie kutafakari tulikotokea na tunapotaka kwenda, turejee maono yake, wosia wake na mawazo yake. Yeye alihubiri sana kuhusu uhuru. Neno uhuru alilitumia katika kauli zake nyingi, aliamini uhuru unaleta maendeleo,” alisema Mwalimu.

Mwalimu alisema kutokana na namna Chadema wanavyothamini maono ya mwasisi huyo wa Taifa, walitumia sehemu ya nukuu zake katika ilani yao hususan uhuru na maendeleo wakichukua maneno yaliyopo kwenye mwongozo wa TANU wa mwaka 1971 ibara ya 28.

“Nyerere aliamini kitendo chochote kinachowapunguzia wananchi uwezo wa kujiamulia mambo yao kinawarudisha nyuma hata kama kinatoa chakula na afya,” alisema Mwalimu.

Alisema Serikali ya wakoloni ilifanya mambo mengi mazuri ikiwamo kujenga barabara, viwanja vya ndege na shule lakini iliondolewa kwa kuwa watu walihitaji uhuru zaidi na si ujira mdogo usiyoongezeka.

(Imeandikwa na Samson Mfalila, Peter Elias, Ephrahim Bahemu na Janet Joseph)