Wakazi Dar wafurika ofisi za Nida kusaka vitambulisho vya uraia

Muktasari:

  • Ili uweze kusajili laini ya simu ni lazima uwe na kitambulisho cha uraia kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida).

Dar es Salaam. Desemba 31, 2019 ndio mwisho wa usajili wa laini za simu kwa alama za vidole.

Ili uweze kusajili laini ni lazima uwe na kitambulisho cha uraia kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida).

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) hadi Agosti, 2019 laini milioni 5.2 ndio zilikuwa zimesajiliwa kati ya laini milioni 44.2.

Leo Jumanne Novemba 12, 2019 Mwananchi limepita katika ofisi za Nida  wilaya ya Ilala na Temeke na kushuhudia idadi kubwa ya wananchi wakisaka vitambulisho hivyo.

Wanaokamilisha taratibu za usajili, hutakiwa kusubiri kati ya wiki sita hadi nane kupata vitambulisho hivyo.

Zimebaki siku 48 kufikia mwisho wa usajili wa laini hizo jambo linaloashiria kuwa baadhi ya wananchi simu zao hazitakuwa hewani kuanzia Januari Mosi, 2020.

Jua kali na foleni haikuwa kikwazo kwa wananchi hao kwani baadhi yao walitumia miamvuli kujikinga na jua huku wauzaji wa juisi, mahindi na maandazi nao wakitumia fursa hiyo kujipatia kipato.

“Sijui walilala hapa maana nimefika saa 12 asubuhi lakini hadi saa 4 asubuhi hata humo (ofisini) sijafanikiwa kuingia hata kusikilizwa ni tabu kwa kweli,” amesema John Issa mkazi wa Mombasa, Gongo la Mboto.

Amesema idadi ya watu katika eneo hilo imezidi kuongezeka kutokana na hofu ya kufungiwa laini za simu ifikapo Desemba 31, 2019.

“Hapa sasa ndio idadi imepungua asubuhi watu walikuwa wengi hadi mlinzi akazuia  wengine kuingia ili kupunguza msongamano. Hata wakielezwa kukaa nje ni kwa muda tu, baadaye wanarudi tena ndani,” amesema, Hawa Hassan mkazi wa Buza.

Amesema mara ya kwanza alijiandikisha  ofisi za Serikali za mitaa lakini hakupata kitambulisho na kulazimika kufika katika ofisi hizo kuulizia.

“Tulipofika hapa tumeambiwa taarifa zetu zimefutika tuanze upya, nimechoka maana hata cheti cha kuzaliwa kimeshapotea inabidi nianze tena kwenda Rita (Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini),” Amesema Hawa.