Wakili ahoji barua ya Kabendera kwa DPP

Muktasari:

Upande wa utetezi katika kesi inayomkabili mwandishi wa habari wa Tanzania, Erick Kabendera umeuomba upande wa mashtaka kueleza lini utakamilisha mchakato wa mteja wao aliyemuandikia barua Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kukiri makosa na kuomba msamaha.

Dar es Salaam. Upande wa utetezi katika kesi inayomkabili mwandishi wa habari wa Tanzania, Erick Kabendera umeuomba upande wa mashtaka kueleza lini utakamilisha mchakato wa mteja wao aliyemuandikia barua Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kukiri makosa na kuomba msamaha.

Umeeleza hayo leo Jumatano Desemba 4, 2019 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwamba ni miezi miwili imepita tangu barua hiyo kwenda kwa DPP.

Hatua hiyo imekuja baada wakili wa Serikali, Ester Martine kuieleza mahakama hiyo kuwa upelelezi bado haujakamilika, ombi la makubaliano si la kutoa uamuzi wa mara moja.

"Jalada lipo ofisi ya DPP na tunakiri kwamba maombi haya yapo hapa kwa miezi miwili natoa ushauri upande wa utetezi afike katika ofisi ya DPP kujua kinachoendelea," amedai Martine

Baada ya maelezo hayo wakili wa utetezi,  Jebra Kambole amedai Oktoba 11, 2019 waliitaarifu mahakama hiyo kuhusu  ombi la makubaliano na DPP, mpaka sasa hawajapata majibu.

"Ni lini watakamilisha mchakato wa makubaliano ya awali na hakuna chochote ambacho kimefanyika, mtuhumiwa yupo gerezani na ni mgonjwa," amedai Kambole.

Hakimu Mkazi Mkuu, Janeth Mtega amesema kufuatia hoja ya upande wa utetezi mahakama inawataka kwenda kwa DPP kufuatilia suala lao.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 18, 2019 itakapotajwa tena.

Katika shtaka la kwanza, Kabendera anadaiwa kujihusisha na mtandao wa uhalifu kwa kutoa msaada kwa genge la uhalifu kwa nia ya kujipatia faida.

 

Shtaka la pili anadaiwa kuwa bila sababu, alikwepa kodi ya Sh173,247,047.02 ambayo ilitakiwa ilipwe Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

 

Katika shtaka la tatu, Kabendera anadaiwa kutakatisha Sh173,247047.02 huku akijua fedha hizo ni zao la kujihusisha na genge la uhalifu na utakatishaji fedha.