Erick Kabendera kuanza majadiliano na DPP

Muktasari:

  • Jebra Kambole, wakili wa mwandishi wa habari nchini Tanzania,  Erick Kabendera ameijulisha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa mteja wake anataka kujadiliana na mkurugenzi wa mashtaka (DPP) namna ya kumaliza kesi inayomkabili.

Dar es Salaam. Jebra Kambole, wakili wa mwandishi wa habari nchini Tanzania,  Erick Kabendera ameijulisha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa mteja wake anataka kujadiliana na mkurugenzi wa mashtaka (DPP) namna ya kumaliza kesi inayomkabili.

Ameeleza hayo leo Ijumaa Oktoba 11, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi mwandamizi, Augustine Rwizile huku wakili wa Serikali,

Wankyo Simon akiieleza mahakama hiyo kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa, upelelezi haujakamilika.

Baada ya Wankyo kueleza hayo,  Kambole  ameijulisha mahakama taarifa kuhusu Kabendera kujadiliana na DPP kwamba ni kwa mujibu wa kifungu namba 194A(2) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2019.

Katika majibu yake, Wankyo amesema jambo hilo ni kweli na wapo katika mchakato, akisisitiza kuwa taratibu zikikamilika wataipa taarifa mahakama.

Kabendera anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka matatu likiwemo la utakatishaji wa zaidi ya Sh173 milioni.

Katika kesi ya msingi,  mshtakiwa anadaiwa katika siku tofauti  kati ya Januari 2015 na Julai 2019 jijini Dar es Salaam alitoa msaada katika genge la uhalifu kwa nia ya kujipatia faida.

Katika shtaka la pili, anadaiwa siku na mahali hapo bila kuwa na sababu za msingi kisheria alishindwa kulipa kodi ya Sh173.24 milioni ambayo ilitakiwa ilipwe kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Katika shtaka la utakatishaji fedha anadaiwa kati ya Januari 2015 na Julai 2019 alijipatia Sh173.24 milioni wakati akizipokea alijua kuwa fedha hizo ni mazao ya makosa tangulizi ya kukwepa kodi na kujihusisha na genge la uhalifu.