Erick Kabendera aieleza mahakama kuhusu matibabu yake

Muktasari:

  • Mwandishi wa habari nchini Tanzania, Erick Kabendera leo Jumanne Oktoba Mosi, 2019 ameielezea Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa anaendelea na matibabu, kwa sasa anatumia dawa.

Dar es Salaam. Mwandishi wa habari nchini Tanzania, Erick Kabendera leo Jumanne Oktoba Mosi, 2019 ameielezea Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa anaendelea na matibabu, kwa sasa anatumia dawa.
Kabendera alifikishwa  mahakamani kwa mara ya kwanza Agosti 5, 2019 akikabiliwa na mashtaka matatu, ambayo ni kuongoza genge la uhalifu, kukwepa kodi na kutakatisha zaidi ya Sh173.2 milioni.
Leo Kabendera amezungumzia matibabu yake mbele ya  Hakimu Mkazi Mwandamizi,  Agustine Rwizile baada ya wakili mwandamizi wa Serikali,  Wankyo Saimon kueleza kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.
Hakimu Rwizile alipotaka ufafanuzi  kuhusu huduma za matibabu, amejibiwa na Kabendera kuwa anaendelea na matibabu.

"Mheshimiwa hakimu ninaendelea na matibabu na ninatumia dawa," amedai Kabendera.
Awali, Kabendera alidai mahakamani hapo kuwa alifanyiwa kipimo cha X Ray kwenye mgongo na uchunguzi wa awali ulionyesha kwenye pingili za mgongo kuna tatizo.
Wakili wa utetezi,  Jebra Kambole aliuomba upande wa mashtaka kuharakisha upelelezi kwa kuwa mshtakiwa yupo ndani, hana dhamana na afya yake bado haijatengamaa.
"Shauri hili lilipokuja mahakamani wakili wa Serikali alidai kuna maeneo machache hawajakamilisha maombi yetu wawe 'serious' kupeleleza shauri hili," amedai Kambole.
Hakimu Rwezile baada ya kusikiliza maelezo hayo ameahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 11, 2019 itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

Katika kesi ya msingi,  mshtakiwa anadaiwa katika siku tofauti kati ya Januari 2015 na Julai 2019 jijini Dar es Salaam, alitoa msaada katika genge la uhalifu kwa nia ya kujipatia faida.
Katika shtaka la pili, inadaiwa siku na mahali hapo mshtakiwa bila kuwa na sababu za msingi kisheria alishindwa kulipa kodi ya Sh173, 247,047.02 ambayo ilitakiwa ilipwe kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Katika shtaka la utakatishaji fedha,  kati ya Januari 2015 na Julai 2019 ndani ya jiji na mkoa wa Dar es Salaam mshtakiwa alijipatia kiasi hicho cha Sh173.2 milioni wakati akizipokea alijua kuwa fedha hizo ni mazao ya makosa tangulizi ya kukwepa kodi na kujihusisha na genge la uhalifu.
SOMA ZAIDI: VIDEO: Mahakama yaelezwa mwandishi Erick Kabendera amepooza mguu mmoja na ana tatizo la kupumua