Masaju aonya mawakili wanaouza haki za wateja

Jaji mkuu wa Tanzania George Masaju akizungumza katika hafla ya kuwapokea Mawakili wapya 449 Jijini Dodoma.
Muktasari:
- Jaji Mkuu wa Tanzania, George Masaju amewapokea mawakili wapya 449 ikiwa ni tukio la kwanza tangu aapishwe kuishika nafasi hiyo na Rais Samia Suluhu Hassan, Juni 15, 2025.
Dodoma. Jaji Mkuu wa Tanzania, George Masaju amewaonya mawakili nchini wenye tabia za kuuza haki za wateja wao kuacha kufanya hivyo, kwa sababu hawatakuwa salama katika maisha yao.
Akizungumza leo Alhamis Julai 3, 2025 wakati wa shughuli ya kupokea mawakili 449, Jaji Mkuu Masaju pia, amewataka mawakili hao kuacha tabia ya kupenda kuishi kwenye miji mikuu ya kama Dodoma na Dar es Salaam kwa kwenda wilayani ambapo kuna fursa nyingi za shughuli waliyoapa kuifanya.
Ametoa mfano wa Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro ambayo ina viwanda, mashamba, machimbo ya madini, hali inayosababisha uhitaji wa huduma za kisheria kutokana na migogoro inayojitokeza.
“Tusijibane sana Dodoma na Dar es Salaam tuangalie maeneo mengine, ninyi mnaopita mikononi mwangu nisingependa mkaharibikiwa nawahakikishia kuwa ni mlezi mzuri.
“Kuliko baadaye tutaanza kuzunguka pale Dar es Salaam, tukaanza ‘ku-behave’ kama vishoka, mkaanza kuuza haki za wateja wetu kama kuna kitu nakichukia katika utumishi wangu ni hicho,”amesema.
Amesema wanapoishi maisha ya hapa duniani, hawawezi kuwa wajanja kwa Mungu.
Masaju ameonya kuhusu mawakili wanaouza haki zawateja wao kwa masilahi binafsi kwamba hawatabaki salama.
“Na sisi tunapenda sana, kununua vigari vidogo vidogo na kutafuta wachumba hatutakuwa na usalama sana. Na watu mnazozipuuza ni zile za wajane, yatima, sisi mahakamani tunaona shida wanazozipata watu katika mashauri ya mirathi, halafu unachukua fedha unasema unapeleka mtoto kusoma India,” amesema.
Amewaomba wasifanye hivyo na badala yake kuwa waadilifu katika katika kazi zao.
Masaju amewataka kuviishi viapo vyao, kutovunja sheria mbalimbali kwa kuwa kufanya hivyo ni kutenda haki kwa Taifa.
“Ushauri wangu ni kwamba mkiishi hiki kiapo muwe na heshima kwa wateja wenu, mahakama na wananchi wa Taifa hili. Kubwa kwenu nyie liwe uwezo na uadilifu. Kuwa na cheti ni tofauti sana na utendaji wa majukumu yako,” amesema.
Masaju amesema uwezo na uadilifu yamekuwa ni changamoto kwenye utumishi wa umma na kuwa hategemei wataenda kuwa kama wanasiasa.
Amesema kuwa mawakili wanaoapishwa na kuwa wanachama wa Chama cha Wanasheria Tanganyika ni watumishi wa umma, hivyo wanawajibika kuzitafsiri sheria kwa usahihi ili kufikia maana halisi iliyokusudiwa ambayo ni kuhakikisha upatikanaji wa haki.
“Uanasheria sio vyeti mlivyopata leo ama mnavyopata huko vyuo vikuu, uanasheria ni utu wako wa kutafasiri vifungu vya sheria, kuna kuitoa tafasiri ya hiyo sheria kwa watu wengine ndio kunaitwa ushauri,”amesema.
Amesema uzoefu wake unaonyesha kuwa wanauwezo wa kutafsiri hizo sheria, lakini kuna udhaifu kwenye mawasiliano ya tafsiri.
Masaju amewataka kujiandaa kuwasaidia wateja wao katika kutafsiri sheria ipasavyo na kama suala haliwezekani waambiwe ukweli badala ya kung’ang’aniza kutaka kupata fedha.
Aidha, amewataka kufahamu kuwa wanapowatetea wateja wa msaada wa kisheria, utetezi wao unatakiwa kuwa sawa na wale ambao wanachukua fedha.
Uchaguzi Mkuu
Pia, Masaju amewataka kutambua kuwa wakati huu wa Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani, wajibu wao mkubwa ni kudumisha utawala wa sheria.
Amewataka wazisome, wazifahamu sheria za uchaguzi ili waweze kuwasaidia vizuri wateja wo wakiwemo wale wagombea wanaotaka wawaongoze kujaza fomu na kuwasaidia kunapotokea migogoro.
Masaju amesema kwa uzoefu wake katika mwaka wa uchaguzi ni mwaka kama wa mavuno kwa mawakili wote na kuwataka kuitumia fursa hiyo vizuri kwa kuwa hapo ndipo watakapopata wateja.
Pia, amewataka kujishughulisha na shughuli za kiuchumi ikiwemo kilimo, biashara na ujasiriamali na kuachana na akili za kizamani kuwa mwanasheria huwezi kufanya shughuli nyingine za kiuchumi ambazo ni halali.
Wakili Godson Kimaro amesema kuwa wao wanaichukulia tukio hilo kama la kihistoria, kwa kuwa ni wa kwanza kuapishwa na Jaji Mkuu mpya.
Ameihakikishia mahakama kuwa watayazingatia na kuyatekeleza kwa umakini yote waliyoelekezwa na Jaji Mkuu.
“Naihakikishia mahakama tunakwenda kufanya kazi kwa weledi ili tuweze kuwasaidia wananchi katika maeneo mbalimbali hapa nchini kupata haki zao,” amesema.
Naye Wakili Julieth Lusiza amesema kuwa watatekeleza kwa dhati maagizo yote waliyopewa na Jaji Mkuu wa Tanzania, akisisitiza kuwa wakili anapopoteza haki ya mteja, hulazimika kutumia gharama kubwa kuitafuta tena katika njia nyingine.
Kwa upande wake, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Chiganga Tengwa amesema kuwa kupokelewa kwa mawakili wapya kumeongeza idadi ya mawakili waliosajiliwa kutoka 12,997 hadi kufikia 13,446.
Sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka sekta ya sheria, wakiwemo Wakili Mkuu wa Serikali, Dk Ally Possi, na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari.