VIDEO: Kabendera: Nimefanyiwa kipimo cha X Ray, damu

Mwandishi wa Habari  za uchunguzi Erick Kabendera akitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

  • Mwandishi wa Habari nchini Tanzania, Erick Kabendera ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu alivyofanyiwa vipiko vya X Ray na damu kwa mara ya kwanza katika Hospitali ya Rufaa ya Amana na amefakanyiwa kipimo cha X Ray kwenye mgongo pamoja na kipimo cha damu.

Dar es Salaam. Mwandishi wa Habari nchini Tanzania, Erick Kabendera ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam kwa mara ya kwanza jana Jumanne Septemba 17, 2019 alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Amana na amefanyiwa kipimo cha X Ray kwenye mgongo pamoja na kipimo cha damu.

kabendera  amesema hayo leo Jumatano Septemba 18, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi mwandamizi Agustine Rwizile baada ya Wakili Mwandamizi wa Serikali Wankyo Saimon kueleza shauri lilikuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Kabendera ambaye ni mwandishi wa habari za ndani na nje ya Tanzania alifikishwa katika mahakama hiyo kwa mara ya kwanza, Agosti 5, 2019 akikabiliwa na mashtaka matatu ambayo ni kuongoza genge la uhalifu, kukwepa kodi na kutakatisha fedha zaidi ya Sh173.2 milioni.

"Nashukuru jana nilifanikiwa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Amana na nilifanyiwa kipimo cha X Ray kwenye mgongo wangu na majibu yametoka," amedai Kabendera.

Kabendera amedai alikuchukuliwa kipimo cha damu na majibu yake bado hajapewa hivyo anaendelea kuvumilia ili majibu hayo yatoke aweze kuanza matibabu.

Pia ameieleza mahakama hiyo kuwa bado ana maumivu makali katika mguu wake jambo kubwa alilokuwa akisubiri ni kupatiwa vipimo ili aweze kuanza matibabu.

Wakili  wa utetezi, Jebra Kambole ameomba ahirisho hivyo shauri hilo litakapokuja wataieleza mahakama hiyo kuhusu majibu ya vipimo vya damu alivyochukuliwa.

Hakimu Rwezile baada ya kusikiliza maelezo hayo ameahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 1, 2019 itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.