Wakili aibua mambo mapya kushikiliwa kwa Kabendera

Mwandishi wa habari, Erick Kabendera

Dar es Salaam. Shilinde Swedy, mwanasheria wa Erick Kabendera anayeshikiliwa tangu Jumatatu iliyopita, amesema polisi walikwenda na mwandishi huyo juzi jioni hadi nyumbani kwake, ambako walimtaka awapatie kadi ya gari na hati ya nyumba.

Wakati Swedy anayetoka Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu, akieleza hayo, kamishna wa uraia na hati za kusafiria wa Idara ya Uhamiaji, Gerald Kihinga amesema kufanya upekuzi na kushikilia kadi ya gari na hati ya nyumba ni sehemu ya upelelezi wao na hakutaka kuzungumzia zaidi suala hilo.

Kabendera, ambaye anaandikia vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi, alikamatwa na polisi akiwa nyumbani kwake Mbweni jijini hapa na Idara ya Uhamiaji imesema inamshikilia kwa ajili ya uchunguzi wa uraia wake.

Akizungumza na Mwananchi jana, Swedy alisema baada ya polisi kufanya upekuzi nyumbani kwa Kabendera, hakupewa dhamana.
“Walifanya upekuzi mara mbili nyumbani kwake na kuchukua kadi ya gari, walitaka na hati ya nyumba lakini walielezwa iko benki,” alisema wakili huyo.

Alisema walipofuatilia Uhamiaji walielezwa kuwa wameshamalizana na Kabendera, lakini polisi bado wanamhitaji kwa mahojiano, lakini Kihinga alisema Uhamiaji bado inamshikilia mwandishi huyo.