Wazee 60+ wakae chonjo, magonjwa haya hatari kwao

Muktasari:
- Ni kweli umri wa uzee ni kihatarishi cha kupata magonjwa lakini mzee mwenye mitindo mibaya kimaisha, yupo katika hatari zaidi ya kupata magonjwa haya.
Kwa Tanzania na nchi nyingine duniani umri wa uzee ni miaka 60 kuendelea. Kitabibu umri huu ni moja ya kihatarishi cha kupata magonjwa yasiyoambukiza.
Sababu ya kimsingi ni kutokana na mchanganyiko wa mambo kadhaa ya kibailojia kama vile kutumika na kulika hatimaye kuchakaa kwa viungo, mrundikano wa mambo ya hatarishi kiafya kadiri umri unavyoenda na uchaguzi usiofaa wa mitindo ya kimaisha.
Magonjwa yasiyoambukiza yanaweza kuathiri ubora wa maisha ya wazee, kuathiri ustawi wao wa kimwili na kiakili, uhuru na tija.
Ni Changamoto kutibu magonjwa haya kwasababu yanahitaji huduma ziinazoendelea kwa muda mrefu.
Ni kweli umri wa uzee ni kihatarishi cha kupata magonjwa lakini mzee mwenye mitindo mibaya kimaisha, yupo katika hatari zaidi ya kupata magonjwa haya.
Mienendo na mitindo mibaya ya kimaisha ni pamoja unywaji pombe, uvutaji tumbaku, ulaji holela wa chumvi, sukari, wanga na mafuta na kutofanya mazoezi au kuushughulisha mwili na kazi.
Magonjwa hayo ni pamoja na shinikizo la juu la damu, unene, matatizo ya mishipa ya damu ya moyo, lehemu nyingi, kiharusi na kisukari.
Vile vile ugonjwa sugu wa figo, matatizo sugu mfumo wa hewa, saratani mbalimbali, matatizo ya viungo vya mwili ikiwamo mifupa na magonjwa ya akili.
Ni muhimu kutumia njia za kujikinga mapema kabla ya kupata magonjwa hayo, hasa kwa wale wanaoelekea uzeeni, ambao tayari ni wazee au tayari wanakabiliwa na magonjwa hayo.
Mazingira bora ya kuishi yasiyo katika mazingira yenye uchafuzi wa hewa na kelele nyingi , lishe bora iliyozingatia kanuni za afya na mazoezi mepesi, ni muhimu kwa afya ya wazee.
Wafanye nini?
Wazee wa umri wa miaka 60+ wanatakiwa kupendelea zaidi kula mbogamboga, matunda, protini itokanayo na mimea, kuepuka chumvi, sukari au wanga na mafuta mengi.
Ni vyema umri huo kuwaona wataalamu wa lishe katika huduma za afya ili kukupa mwongozo mpana na ratiba ya vyakula.
Mzee kufanya mazoezi huwa ni vigumu, kwa yule anayeweza kutembea vyema kufanya zoezi la kutembea angalau hatua 10,000 kwa siku au umbali wa kilometa mbili kwa dakika 30 kwa siku katika siku 5 za wiki.
Au unaweza kujishughulisha na kazi za nyumbani kama kufanya kazi za bustani au usafi wa nyumba na mazingira.
Kingine wanachoweza kufanya ni kulala angalau saa nane kwa usiku mmoja, kupata mapumziko na kupata burudani ili kuepukana na matatizo ya akili.
Wafanye uchunguzi wa afya wa jumla mara moja kwa miezi sita, hii inasaidia kubaini matatizo ya kiafya mapema kwa gharama ndogo.