VIDEO: Mwandishi wa habari Erick Kabendera arudishwa rumande kwa siku 12

Muktasari:

Mashtaka yanayomkabili Kabendera ni kupanga na kushiriki mtandao wa uhalifu, kukwepa kodi zaidi ya Sh173 milioni na utakatishaji fedha zaidi ya Sh173 milioni

Dar es Salaam. Kesi inayomkabili mwandishi wa habari za uchunguzi nchini Tanzania, Erick Kabendera imeahirishwa kutokana na hakimu mkazi mwandamizi, Augustine Rwizile kupata udhuru.

Mbali na hakimu huyo kupata udhuru, wakili wa Serikali mwandamizi, Wankyo Simon ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Simon ameeleza hayo leo Jumatatu Agosti 19, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Agustina Mmbando

“Hakimu anayesikiliza shauri hili  ambaye ni hakimu mkazi mwandamizi, Augustine Rwizile amepata udhuru,” amesema Simon.

Wakati Simon akieleza hayo, wakili wa Kabendera, Jebra Kambole ameutaka upande wa mashtaka kuhakikisha upelelezi wa shauri hilo unakamilika kwa wakati kutokana na mteja wake kutokuwa na dhamana.

"Hatuna  pingamizi kuhusu kupata udhuru kwa hakimu, ila  tunaomba upande wa mashtaka wajitahidi kukamilisha upelelezi kwa wakati ili kesi hii iweze kuendelea kwa sababu mteja  wangu anaendelea kusota rumande kutokana na mashtaka yanayomkabili kutokuwa na dhamana,” amesema Kambole.

Hakimu Mmbando baada ya kusikiliza hoja za upande zote ameahirisha kesi hiyohadi Agosti 30, 2019 itakapotajwa tena.