Makonda: Elimu ya fedha itajenga jamii imara
Muktasari:
- Asema elimu ya fedha si muhimu kwa wateja wa benki pekee, bali kwa Watanzania wote, kwani huwasaidia kupanga matumizi, kuwekeza kwa usahihi na kuepuka kupoteza mitaji kutokana na ukosefu wa taarifa.
Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda amesema elimu ya fedha kwa wananchi inasaidia kujenga jamii yenye uwezo wa kufanya maamuzi sahihi ya kifedha na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Amesema elimu hiyo si tu muhimu kwa wateja wa benki pekee, bali kwa Watanzania wote, kwani huwasaidia kupanga matumizi, kuwekeza kwa usahihi na kuepuka kupoteza mitaji kutokana na ukosefu wa taarifa.
Makonda amesema hayo leo, Jumatano Julai 22, 2026, wakati wa uzinduzi wa msimu wa nne wa kipindi cha Zogo Mchongo, ambacho ni sehemu ya mkakati wa Benki ya CRDB wa kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya fedha, katika kipindi ambacho matumizi ya teknolojia na huduma za kidijitali yanaongezeka.
"Kwa elimu mnayoitoa, hawanufaiki wateja wenu pekee bali jamii nzima ya Watanzania. Jamii yetu ikielimika, naamini uchumi nao utakua zaidi kwa sababu watu watakuwa na uwezo wa kuwekeza kutokana na taarifa sahihi walizonazo, hivyo kuepuka kupoteza mitaji yao," amesema Makonda.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk Abdulmajid Nsekela, amesema pamoja na kasi ya maendeleo ya teknolojia, huduma za kidijitali na matumizi ya Akili Unde (AI), elimu ya fedha imeendelea kuwa msingi muhimu wa kuwawezesha wananchi kutumia huduma hizo kwa usalama na manufaa.
"Kadri dunia inavyozidi kuwa ya kidijitali, ndivyo umuhimu wa elimu ya fedha unavyozidi kuongezeka. Huduma za kifedha zinapokuwa rahisi kufikiwa, wananchi wanahitaji maarifa zaidi ya kuzitumia kwa busara," amesema.
Amesema kwa CRDB, ujumuishi wa kifedha hauishii kuongeza idadi ya watu wanaotumia huduma za benki pekee, bali pia kujenga jamii yenye uwezo wa kupanga matumizi, kuweka akiba, kuwekeza, kukopa kwa uwajibikaji na kuboresha ustawi wa kifedha wa familia na taifa.
Dk Nsekela amesema kupitia kipindi cha Zogo Mchongo, benki hiyo imefanikiwa kuyafikia makundi mbalimbali ya Watanzania kwa kutumia mtindo unaounganisha elimu ya fedha, burudani na teknolojia.
Amesema msimu huo utakuwa na vipindi vinane vitakavyorushwa kupitia Clouds TV na kupatikana katika majukwaa ya kidijitali ya Benki ya CRDB, vikilenga kuwajengea wananchi uwezo wa kufanya maamuzi bora ya kifedha katika maisha yao ya kila siku.
Katika hatua mpya ya ubunifu kwenye msimu huu, Benki ya CRDB imemtambulisha 'Elle', msaidizi wa kidijitali anayewakilisha matumizi ya Akili Unde katika utoaji wa elimu ya fedha.
Dk Nsekela amesema hatua hiyo inaonyesha dhamira ya Benki ya CRDB ya kutumia teknolojia kukuza maarifa na kuongeza ufanisi wa utoaji wa elimu kwa wananchi.
Aidha, kipindi hicho kitatoa mwanga kuhusu namna Watanzania wanavyoweza kunufaika na fursa za kiuchumi zitakazotokana na matukio makubwa ya kimataifa, yanayotarajiwa kufanyika nchini mwakani, ikiwemo michuano ya AFCON na mashindano ya ulimbwende ya Miss World, kwa kuwasaidia kutambua na kutumia fursa za biashara na uwekezaji.
"Tunataka elimu ya fedha isiwe jambo linaloishia kwenye kipindi cha televisheni pekee, bali iwe sehemu ya tabia na maamuzi ya kila siku ya Mtanzania," amesisitiza.
Benki ya CRDB imewaalika Watanzania wote kufuatilia vipindi vya msimu huu mpya, kushirikisha familia na marafiki zao, na zaidi ya yote kutumia maarifa watakayoyapata kujenga ustawi wao wa kifedha na kunufaika na fursa za uchumi wa kidijitali.