Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Samia ataka nchi za Afrika zijitegemee sekta ya afya

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza katika Mkutano Maalum wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) kuhusu afya leo Jumatano Julai, 2026 katika hoteli ya Elisa, jijini Accra, Ghana.

Muktasari:

  • Rais ametoa wito huo leo Julai 22,2026 wakati akihutubia mkutano maalumu wa wakuu wa nchi na serikali wa Umoja wa Afrika kuhusu afya uliofanyika jijini Accra Ghana.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amezitaka nchi za Afrika kuongeza uwekezaji wa ndani katika sekta ya afya ili kujenga mifumo imara, endelevu itakayojitegemea katika usimamizi wa sekta hiyo.

Taarifa iliyotolewa leo Julai 22,2026 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bakari Machumu imeeleza kuwa Rais Samia ametoa wito huo akihutubia mkutano maalumu wa wakuu wa nchi na serikali wa Umoja wa Afrika kuhusu afya uliofanyika jijini Accra Ghana.

Mkutano huo umejadili namna ya kuharakisha utekelezaji wa ajenda ya afya ya Afrika kupitia usawa katika upatikanaji wa huduma, afya kwa wote, kutokomeza Ukimwi, kuboresha afya ya mama na mtoto, pamoja na kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza na yasiyopewa kipaumbele.

Rais Samia amesema Tanzania  imeanza kutekeleza ramani ya afya ya Umoja wa Afrika 2030 kwa kuiingiza katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano wa 2026/2027 –2030/2031, huku ikijielekeza kwenye uwekezaji katika uzalishaji wa dawa, kuimarisha mifumo ya afya na kuongeza uwezo wa nchi kujitegemea katika huduma za afya.

“Afrika ina maarifa, rasilimali watu na uwezo wa kubadili mifumo yake ya afya. Tunachohitaji sasa ni utashi mkubwa wa kisiasa, uwekezaji wa ndani na mshikamano wa bara,” amesema Rais Samia.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akishiriki Mkutano Maalum wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) kuhusu afya, jijini Accra, Ghana.

Mbali na hilo, Rais Samia amesema Serikali imefanya mageuzi ya sera na sheria ili kuvutia uwekezaji na kurahisisha biashara, hatua zilizowezesha kuanzishwa kwa viwanda 13 vya uzalishaji dawa huku wawekezaji 149 wakionesha nia ya kuwekeza nchini.

Aidha, Rais Samia amesema Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) imekuwa ya kwanza barani Afrika kufikia kiwango cha tatu cha ukomavu wa mifumo ya udhibiti wa hatua inayotarajiwa kuharakisha uzalishaji wa dawa bora na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje.

Rais Samia amesema Serikali imeongeza bajeti ya sekta hiyo kutoka Sh1.8 trilioni mwaka 2024/25 hadi Sh3.1 trilioni mwaka 2026/27, sambamba na kuanzisha bima ya afya kwa wote ili kuwawezesha wananchi, wakiwemo wenye kipato cha chini, kupata huduma muhimu za afya kwa gharama nafuu.

“Uwekezaji huo umewezesha kujengwa kwa hospitali za wilaya 119, vituo vya afya 649 na zahanati zaidi ya 2,700, na kuongeza idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya kutoka takribani 10,000 hadi 13,700 kufikia Machi, 2026,” amesema Rais Samia.

Amesema maboresho hayo yamechangia ongezeko la uzazi unaofanyika katika vituo vya afya kutoka asilimia 65 hadi 86, na uzazi unaohudumiwa na wataalamu kutoka asilimia 66 hadi 85.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Ghana, John Mahama, Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) ambaye pia ni Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye, pamoja na viongozi mbalimbali waliohudhuria hafla ya ufunguzi wa mkutano maalumu wa Umoja wa Afrika kuhusu afya.

Rais Samia amesema maboresho hayo, pia yamechangia kupungua kwa vifo vya watoto chini ya miaka mitano kutoka 147 hadi 43 kwa kila vizazi hai 1,000; na vifo vya kina mama vitokanavyo na uzazi vikipungua kutoka 556 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000.

Akifungua mkutano huo, Rais wa Ghana, John Dramani Mahama, amesema kupungua kwa ufadhili wa afya duniani kunapaswa kuwa fursa kwa Afrika kuongeza uwekezaji wa ndani na kujenga mifumo ya afya inayojitegemea.

Katika hotuba yake, Rais Mahama ameahidi kumuunga mkono Rais Samia katika utekelezaji wa jukumu lake la kinara wa Umoja wa Afrika wa afya ya uzazi, mama na mtoto, akisema uongozi wake utasaidia kuharakisha maendeleo katika eneo hilo.

Naye, Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika na Rais wa Burundi, Évariste Ndayishimiye, amezitaka nchi wanachama kuongeza uwekezaji katika huduma za afya za msingi na kuimarisha uwezo wa bara la Afrika wa kuzuia, kugundua na kukabiliana na milipuko ya magonjwa.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema maazimio ya mkutano huo yatakuwa na maana ikiwa yatafuatiwa na utekelezaji madhubuti, akisisitiza kuwa hatua zinazochukuliwa sasa zitakuwa msingi wa mustakabali wa afya barani Afrika.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Mahmoud Ali Youssouf, ametoa wito kwa nchi wanachama kuharakisha ujenzi wa mnyororo wa uzalishaji wa bidhaa za afya barani Afrika ili kuongeza upatikanaji wa dawa, chanjo na vifaa tiba na kuimarisha usalama wa afya wa bara.